Dondoo

Kisura atolewa uzuzu na mama ya kalameni

December 17th, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

Kiomo, Kitui

Kalameni mmoja kutoka eneo hili alijipata pabaya baada ya mama yake kumkemea vikali kwa kumhadaa kipusa kwamba hakuwa ameoa.

Inasemekana mama ya jamaa alichukua hatua hiyo baada ya kupata habari kwamba mwanawe alitumia udanganyifu ili kumuoa mke wa pili.

Kulingana na mdokezi, polo alikuwa ameoa mke wa kwanza na duru zinasema alikutana na kipusa mwingine na akavutiwa na urembo wake.

Inasemekana jamaa alilazimika kumdanganya kwamba hakuwa ameoa na hakuwa na watoto nje ya ndoa. Aliposikia hivyo, kipusa alinaswa na hadaa za polo na wakaanza mipango ya kuoana mara moja.

Kulingana na mdokezi, mambo yalimuendea vibaya jamaa huyo wakati mwanadada alipomtembelea bila kumfahamisha na akakutana na mama yake.

“Habari mama. Mimi ni mpenzi wa mwanao. Nimekuja kumtembelea na pia tujuane kwa vile tunapanga kuoana,” mrembo alimueleza mama ya jamaa.

Mama ya polo alipigwa na butwaa.

“Unakubali kuwa mke wa pili?” mama alimuuliza kipusa ambaye alibaki mdomo wazi aliposikia maneno hayo. ? “Mimi aliniambia bado hajaoa na tena hana mtoto yoyote nje ya ndoa,” mwanadada alisema. ? Duru zinasema mama aliandamana na kipusa hadi kwa nyumba ya polo na kumkuta akiwa na mkewe. ? “Unamjua huyu msichana?” polo aliulizwa. Polo alibaki amenyamaza.

“Mbona unamdanganya kuwa hujaoa ilhali una familia,” mama alianza kumfokea polo. ? Polo alitamani ardhi immeze.

“Kichwa chako ni kizuri kweli. Unawezaje kukana mkeo. Una shida gani wewe ama umerogwa,” mama aliwaka.

Mama alilazimika kumshauri mwanadada. “Achana na huyu. Ni kama hana akili. Tafuta mwanamume mwingine atakayekuoa,” alimweleza mwanadada.