Makala

Kiswahili kutumika bungeni

November 22nd, 2020 2 min read

Na WANGU KANURI

MIJADALA bungeni itakuwa ikiendeshwa kwa Kiswahili kila Alhamisi, aghalabu kwa mbunge anayejisikia kufanya hivyo.

Mwelekeo huu umenuia kufufua mtazamo wa aliyekuwa rais wa kwanza nchini Kenya Jomo Kenyatta. Licha ya mwelekeo huu kufanya bunge kuwa jukwaa la kichekesho miaka 46 iliyopita, Rais Uhuru Kenyatta alisema Alhamisi wiki jana alikubali Kiswahili kitumike bungeni.

Itakumbukwa kuwa mara ya kwanza Kiswahili kutumika bungeni, wabunge walitatizika kujieleza kwa lugha hiyo huku macho yakielekezewa wabunge wa sasa. Kupitia rekodi zilizoko bungeni, mara ya kwanza Kiswahili kutumika kama lugha ya mawasiliano ilikuwa Julai 4, 1974.

Rais Jomo Kenyatta alifikia mwelekeo huu baada ya mkutano na wanachama wa kitaifa wa Kanu ambao walipinga kukitumia Kiswahili bungeni. Haikuwa rahisi kwa mwanasheria mkuu Charles Njonjo ambaye amekolea katika lugha ya Kiingereza huku rais Kenyatta akimsisitizia kuwa sharti ajieleze kwa Kiswahili.

Katika miaka ya kwanza baada ya kupata ukoloni, wabunge walitaka Kiswahili kutumika bungeni ili kudumisha utamaduni wa nchi. Siku moja baada ya rais Kenyatta kutenga siku rasmi ya kuzungumza Kiswahili bungeni wabunge walitatizika kujieleza katika mjadala kuhusu ajenti wa kuangazia suala la mashamba nchini.

Spika wakati huo bwana Fred Mati aliwaeleza wabunge kuwa hawakuwa na lingine bali kufuata amri ya rais.

“Ninatangazo kuu. Nimezungumza na rais kuhusu suala la kubadilisha lugha ya kuwasiliana bungeni kutoka Kiingereza hadi Kiswahili,” kumbukumbu za rekodi za bunge July 15, 1974. Akaongeza kwa kusema, “Nimemweleza changamoto tutakazopitia lakini anaonelea tuanzie mara moja, huku tukipiga hatua za kuboresha mazungumzo yetu baadaye.

Spika Mati akamwamrisha mbunge aliyekuwa anafuata mbunge wa Kilungu Mutiso Muyu kuzungumza bunge kwa Kiswahili. Mbunge wa Butere Martin Shikuku anayefuata kikamilifu kanuni za bunge, alilalamikia amri hiyo geni kutoka kwa Rais huku akipendekeza bunge kusimamisha kwanza amri hiyo.

Hata hivyo, aliyekuwa waziri msaidizi wa wizara ya ardhi na makazi, G. Kariuki, alisema kuwa, “Rais yu juu ya sheria. Sasa ameamua tutumie Kiswahili.” Waziri wa ujumbe na mawasiliano bwana Robert Matano, alikuwa miongoni mwa waliosukuma kujulikana na kutumiwa kwa Kiswahili kwani alikienzi Kiswahili na aliweza kujieleza pasi tatizo.

Siku hiyo wabunge walitatizika wakijaribu kuchagua neno mwafaka la misamiati ya Kiingereza huku mbunge wa Kikuyu, JK Gatuguta akitaka kujua ni neno gani mwafaka la kutumia ili kusema ‘point of order’ na jinsi ya kumwita spika; msemaji ama mwenyekiti lakini hakuna aliyekuwa na jibu.

Kwa mfano mbunge mmoja alisema kuwa alitaka kujua mbona wakazi wa eneo lake walicheleweshwa kupatiwa stakabadhi zao za shamba na wizara ya ardhi huku wizara hiyo ikiwapa ahadi za mwezi ujao.

GG Kariuki alimjibu: kwa Kiswahili mwezi ujao ni sawa sawa na ‘as soon as possible’ katika lugha ya Kiingereza. Mbunge mwingine aliyekuwa na maoni tofauti akasema, “Sijui kama hiyo ndiyo tafsiri sahihi ama inaafikiana tu na wizara hiyo.”

Mbunge George Anyona alilalamika kuwa hakuweza kujieleza kwa Kiswahili huku mbunge wa Makuyu, Wachira Waweru akishindwa kusema jina la dawa ambayo ilikuwa inakosekana katika hospitali za eneo bunge lake kwa kuwa hakujua jina la dawa hiyo kwa Kiswahili. Mbunge wa Kisumu ya Kati, bi Grace Onyango kwa utani akamweleza bwana Waweru kujieleza kwa lugha yake ya mama ambapo alipoanza kujieleza wabunge wakaangua kicheko. Bwana Njonjo alishindwa kuelewa alichosema Waziri Ronald Ngala huku ikimlazimu kurudia swali lake kwa Kiingereza.

Kwa wabunge waliochanganya ndimi, spika akawaamuru kusita kufanya hivyo. Hata hivyo, kilichoandikwa katika kitabu kinachowekwa ripoti za jinsi mijadala ya bunge inavyoendeshwa kilikuwa na maandishi ya kutatanisha.

Baada ya mwaka 1974, bunge ilibatilisha katiba huku Kiingereza na Kiswahili zikifanywa lugha rasmi za mawasiliano katika bunge. Rais Kenyatta alipozungumza kwa Kiswahili, vituo vyote vya uanahabari vikapeperusha maneno yake.