Kimataifa

Kiswahili sasa kufundishwa nchini Afrika Kusini

September 18th, 2018 1 min read

BBC na PETER MBURU

PRETORIA, AFRIKA KUSINI

LUGHA ya Kiswahili sasa itaanza kufundishwa kama somo la kuchagua katika shule za Afrika Kusini kuanzia mwaka 2020 kama mbinu ya ‘kuunganisha Afrika’, wizara ya elimu nchi hiyo imesema.

Akitoa ujumbe huo, Waziri wa Elimu Angie Motshekga (pichani) alisema hiyo itakuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kutoka nje ya taifa hilo kufundishwa shuleni.

Kati ya masomo mengine yanayotolewa kama ya kuchaguliwa ambayo ni lugha za kutoka nje ya taifa hilo ni Kifaransa, Kijerumani na Kimandarin.

Bi Motshekga alisema Kiswahili ndiyo lugha ya Kiafrika inayozungumzwa zaidi humu barani baada ya Kizungu na Kiarabu na “iliyo na uwezo wa kupenyeza katika mataifa ambayo hayaitumii na ina nguvu ya kuwaleta Waafrika pamoja.”

“Pia ni moja ya lugha rasmi za Umoja wa Afrika. Tuna hakika kuwa kufunzwa kwa Kiswahili katika shule za Afrika Kusini kutasaidia kuunganisha jamii yetu na nyingine za Kiafrika,” akasema Bi Motshekga.

Hatua hii imekuja miezi miwili baada ya kiongozi wa upinzani nchini humo Julius Malema kupendekeza kuinuliwa kwa Kiswahili kuwa lugha ya mawasiliano barani, kama mbinu moja ya kujikomboa kutokana na lugha za kigeni.

Bw Malema alipendekeza kuwepo kwa lugha moja ya kutumika katika bara zima, akisema Kiswahili ndiyo lugha pekee iliyosimama kuchukua nafasi hiyo, mbali na kuwa na Rais mmoja wa bara na wabunge wa bara.

“Lazima tuwe na lugha inayowaunganisha Waafrika, kisha tuachane na kuzungumziana wenyewe kwa wenyewe tukitumia Kizungu,” akasema Bw Malema.