Habari

Kitabu chenye mada zinazohusu ICC na changamoto ya uhalifu barani Afrika chazinduliwa

August 23rd, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KITABU kipya chenye mada zinazohusu Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa (ICC) na ambacho vilevile kinamulika changamoto ya uhalifu barani Afrika kimezinduliwa.

Hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho imehudhuriwa na mwakilishi wa balozi wa Uholanzi nchini Bi Kirsten Hommes, Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) Prof Paul Wainaina, wahadhiri wakuu wa chuo hicho na wadau wengine muhimu waliochangia kukamilika kwa kitabu hicho.

Kitabu hicho kilichopewa anwani ‘International Criminal Justice In Africa Since The Rome Statute’ kimezinduliwa Ijumaa katika chuo hicho cha KU ambapo kimepigiwa chapuo na watu wengi.

Kinaangazia na kujadili kwa kina mada na maswala nyeti.

Wasomi kadha walitoa mchango wao kuhusu umuhimu wa kudumisha amani na kutenda haki kwa wananchi ili kuepukana na machafuko yanayoshuhudiwa kila mara barani Afrika.

Bi Hommes amesema cha muhimu kwa viongozi katika nchi za bara Afrika ni kutendea watu haki popote walipo na kuhakikisha kuna usawa.

Amekisifia kitabu hicho kipya kwa kusema kimeangazia maswala mengi kuhusu jinsi haki inavyostahili kutendewa kila mmoja bila kubagua.

Ametoa wito kwa watu kukisoma kitabu hicho ili kuelewa jinsi kesi zinavyoendeshwa kule The Hague, Uholanzi ambako ndiko yaliko makao makuu ya ICC na jinsi viongozi wanavyostahili kuepuka kusafirishwa hadi huko kwa tuhuma za mauaji ya halaiki katika nchi zao.

Naibu Chansela wa KU Prof Wainaina amekosoa viongozi wa mataifa ya bara Afrika ambao hukiuka sheria iliyowekwa kimataifa huku wakijifanya kutaka hiyo sheria itekelezwe kwa mwananchi wa chini.

“Ni vyema sheria zilizowekwa zifuatwe kikamilifu na kila mmoja ili haki iweze kutekelezwa ipasavyo. Tungetaka sisi wote tuwe sawa chini ya sheria,” amesema Prof Wainaina.

Amesema kuna nchi pia za nje ambazo hazitaki kufuata sheria za kimataifa na kanuni za ICC huku zikitaka mzigo wa makosa uwasilishwe au ubebwe na mataifa ya bara Afrika.

Pongezi

Amewapongeza wote waliochangia kwa njia moja ama nyingine kufanikisha kuchapishwa kwa kitabu hicho hasa wahariri na waandishi.

“Kazi mliofanya ni muhimu na itaweza kuelimisha watu wengi kuhusu jinsi ya kufuata sheria na kutendea watu haki bila kutumia fujo katika kutatua changamoto zilizopo,” amesema Prof Wainaina.

Hata hivyo, amesema kitabu hicho kinastahili kufanyiwa uchunguzi wa kila mara ili kuja na mawazo mengine mapya kuhusiana na mahakama hiyo ya ICC.

Pia amependekeza kuwe na hafla za kila mara kujadiliana mengi kuhusu maswala ya ICC ili kuja na mawazo tofauti.

Dkt Faith Kabata ambaye pia alitoa maoni yake amesema ni vyema viongozi wa Afrika wawe wakiheshimu sheria ya kimataifa ili kutendea wananchi haki.

“Sheria inastahili kufuatwa na kila mmoja. Hakuna haja ya watu wa kiwango cha chini kunyanyaswa huku wakubwa wakiepuka hiyo sheria,” amesema Dkt Kabata.