Habari MsetoSiasa

#KITAELEWEKA: Ngunjiri amlaumu Ruto wabunge wa Bonde la Ufa kumgomea Uhuru

October 23rd, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

MBUNGE mtatanishi wa Nyeri mjini Ngunjiri Wambugu amemlaumu naibu wa Rais William Ruto kufuatia hatua ya wabunge wa eneo la Bonde la Ufa kuondoka kutoka mkutano wa Rais Uhuru Kenyatta, akisema wanajaribu kumlazimisha Rais kuimba wimbo wa Ruto.

Bw Wambugu, ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa naibu wa Rais aliendeleza kampeni yake ya #Kitaeleweka, akikosoa hatua ya wabunge hao kuwa ilikuwa ukosefu wa heshima kwa Rais Kenyatta.

Vilevile, alimkosoa Bw Ruto kwa kukosa kuzungumzia suala hilo licha ya kuwa lilihusisha viongozi wa eneo lake.

Kupitia akaunti yake ya Facebook Jumanne, mbunge huyo alisema viongozi wa Bonde la Ufa wamekuwa wakimsukuma Rais kutangaza mwelekeo wa kisiasa licha ya kuwa alisema hataki siasa hadi 2022 itakapofika.

“Wakati wabunge wa Bonde la Ufa wanamkosea Uhuru heshima, tunatazama,” akaanza.

“Kwanza wabunge wa #TangaTanga walimlazimisha Rais kutangaza kuwa anamuunga mono Ruto 2022 licha ya kuwa hajawahikataa maneno yake kumhusu Ruto. Uhuru amesisitiza kuwa hatakuwa sehemu ya siasa zozote hadi atakapomaliza kazi.

Wabunge hawa kujaribu kumlazimisha Uhuru kupiga siasa licha ya kuwa amesema hatafanya hivyo machoni na mbele ya umma inaonekana. DP Ruto hajasema chochote kuhusu kitu ambacho wazi ni ukosefu wa heshima kwa Rais na vikosi vyake.

Siku inayofuata wanaondoka kutoka hafla nyingine ya Uhuru. Wanasema ni kwa ajili ya Gavana Laboso lakini hafla sio ya Laboso, ni ya Uhuru,” Bw Wambugu akasema.

Mbunge huyo alifunga kwa kusema hatua ya viongozi hao ni ishara ya kile kinawezakufanyika ikiwa Bw Ruto atachukua Urais 2022, akisema hilo halitafanyika.

“Ikiwa watu hawa wanamkosea Uhuru heshima akiwa Rais, na akistaafu je, wakipata Urais? #Kitaeleweka,” akaandika.