Michezo

KITANUKA: Liverpool yaalika Newcastle

September 14th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

MABINGWA mara 18 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Liverpool wanatarajiwa kuendeleza ukatili wao watakapoalika Newcastle uwanjani Anfield leo Jumamosi kwa dhamira ya kukwamilia uongozi ili kuimarisha juhudi za kumaliza ukame wa miaka 29 bila taji la ligi.

Vijana wa kocha Jurgen Klopp wamezoa ushindi katika mechi nne za kwanza na kufungua mwanya wa alama mbili dhidi ya mabingwa watetezi Manchester City.

Kasi ya kutisha ya mabingwa hao wa Klabu Bingwa Ulaya iliichoma Norwich, Southampton, Arsenal na Burnley; onyo kuwa wako makini zaidi kurekebisha walikokosea pembamba kuvua City ya kocha Pep Guardiola taji msimu uliopita.

City itakuwa na kibarua kigumu kuzuia Liverpool inayojivunia washambuliaji matata Sadio Mane, Mohamed Salah na Roberto Firmino, kushinda EPL kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 1990.

Vijana wa Guardiola walishinda ligi kwa mwaka wa pili mfululizo msimu uliopita baada ya kutetemesha wapinzani, lakini Liverpool inaonekana bora zaidi msimu huu wala Newcastle haitarajiwi kupunguza moto huo.

Newcastle inazuru Anfield bila ushindi katika mechi tano dhidi ya Liverpool ikiwemo kulimwa katika tatu zilizopita.

Mara ya mwisho Newcastle iliposhinda Liverpool ligini uwanjani Anfield ilikuwa 2-0 mwaka 1994.

Vijana wa kocha Steve Bruce wanashikilia nafasi ya 14 wakijivunia ushindi mmoja msimu huu waliposhangaza Tottenham kwa bao 1-0 mnamo Agosti 25.

Huku City ikiratibiwa kuchuana na Norwich baadaye leo, vijana hawa wa Guardiola huenda wakajipata alama tano nyuma ya Liverpool mechi itakapoanza uwanjani Carrow Road.

Norwich pia inatarajiwa kuwa na kibarua kigumu dhidi ya City, ambayo haijapoteza dhidi yao katika mechi tano zilizopita.

City inayojivunia wachezaji nyota kama Raheem Sterling na Sergio Aguero haijapoteza mechi msimu huu baada ya kupepeta West Ham, Bournemouth na Brighton. Hata hivyo, sare ya mabao 2-2 dhidi ya Tottenham ilitosha kuhakikishia Liverpool uongozi na itakuwa makini kuepuka kuteleza tena dhidi ya Norwich inayokaribia mkiani.

Nayo Manchester United ya kocha Ole Gunnar Solskjaer inaweza kuota tu kushindania taji baada ya mwanzo mbaya kuonyesha jinsi ilivyopoteza makali.

Beki Harry Maguire

United, ambayo itaalika Leicester uwanjani Old Trafford leo Jumamosi jioni, imeandikisha ushindi mmoja katika mechi nne za kwanza, ikitumai beki mpya Harry Maguire ataipa msukumo kuipiga klabu hiyo yake ya zamani.

Maguire ni beki ghali duniani baada ya kujiunga na United kwa Sh10.2 bilioni, lakini mchezo wa Muingereza huyu dhidi ya Kosovo katika mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Bara Ulaya ulionyesha bado hajaiva.

Leicester na United zinashikilia nafasi za tatu na nane, mtawalia. Hata hivyo, United inajivunia rekodi ya kutoshindwa na Leicester katika mechi 10 na italenga kuiimarisha.

Kocha Mauricio Pochettino atatumai kufungwa kwa kipindi kirefu cha uhamisho cha Bara Ulaya kutaimarisha ari ya wachezaji wake wa Tottenham, ambao wataalika nambari nne Crystal Palace wakiwinda ushindi wa pili.

Pochettino alikuwa na wasiwasi kuhusu wachezaji wake kadhaa kuhama katika kipindi hicho akiwemo Christian Eriksen.

Naye mshambuliaji wa Chelsea, Tammy Abraham ataingia katika vitabu vya kumbukumbu kwa kuwa mchezaji wa tatu aliye na umri wa miaka 21 ama chini kufunga mabao mawili ama zaidi katika mechi tatu za EPL baada ya Cristiano Ronaldo na Dele Alli, ikiwa atafunga mabao mawili dhidi ya Wolves.