Habari

Kitany: Nimempoteza bavyaa

September 3rd, 2019 2 min read

Na SAM KIPAGAT

KESI ya kutaka talaka aliyowasilisha Bi Marianne Kitany dhidi ya Seneta wa Meru, Mithika Linturi imechukua mkondo mpya baada ya kifo cha babake seneta huyo mnamo Jumatatu.

Mapema Jumanne, Bi Kitany ameiambia mahakama kwamba hayuko tayari kuendelea na kesi kwa sababu anaomboleza kwa kumpoteza “bavyaa” yaani baba ya ‘mume wake’.

Kupitia kwa wakili wake Danstan Omari, Bi Kitany amesema huu ni wakati wa majonzi na anapanga kusafiri hadi Igembe kushiriki katika mipango ya mazishi.

“Kwa niaba ya mlalamishi, hatuko tayari kuendelea. Amempoteza bavyaa, aliyefariki jana (Jumatatu) usiku. Anapitia kipindi kigumu na anapanga kuenda Meru kuwa sehemu ya familia na jamaa kwa ajili ya kushirikiana katika mipango ya kumzika mwendazake,” amesema Wakili Omari.

Akaongeza: Nina ujumbe mzito kutoka kwake. Aidha, anatuma salamu za pole kwa mumewe na watu wote wa Igembe.”

Amebainisha kwamba mteja wake atakuwa tayari kuendelea na kesi mara baada ya mazishi.

“Anakwenda (Linturi) kinyume na utaratibu wa Kiafrika kusisitiza kesi iendelee. Mteja wangu ameathirika sana kihisia baada ya kumpoteza bavyaa,” akaongeza.

Hata hivyo, mawakili wa Linturi— Muthoni Thiankolu na Prof George Wajakoyah— wamepinga kucheleweshwa kwa kesi wakisema mteja wao yuko tayari.

“Ni vigumu kuzungumzia kifo, na ni vibaya zaidi kutumia kifo kama kisingizio mahakamani kwa kesi ambayo tayari inaendelea,” amesema Bw Thiankolu ambaye amekosoa madai ya Bi Kitany eti marehemu Linturi (mkubwa) ni baba mkwe.

“Ikiwa Linturi mkubwa ni bavyaa wa mlalamishi ni suala la kusikilizwa na kuamuliwa. Maagizo niyopata kutoka kwa mteja wangu ni kwamba kesi inafaa kuendelea,” amesema.

Bw Thiankolu amesema seneta anaona kwamba kuchelewesha kesi kunamuumiza na kuharibu mipango yake.

“Ni kichekesho mlalamishi kulia na kujiinamia zaidi ya mtu aliyefiwa,” amesema.

Na kupitia Prof Wajakoyah, Linturi amesema babake akiwa hai alikuwa amekasirika baada ya Bi Kitany kudai alimjengea nyumba wakati akiwa na vijana wa kiume na mabinti.

“Hata kuyafanya mambo kuwa mabaya zaidi, mwanamke huyo ni wa kutoka kabila lingine wakati mzee alikuwa na watoto wa kiume wenye uwezo. Madai yake yalikuwa ni sakata hasa kwa mzee wa Kimeru ambaye ni Njuri Ncheke,” amesema.

Wakili Omari akajibu: “Kama ni ukweli mzee alishtushwa kwamba ni Bi Kitani aliyemjengea nyumba, basi inasikitisha na jambo la kujutia.”

Hakimu Mkuu Peter Gesora amesema hatajiingiza kwa suala hilo kwamba Bi Kitany alikuwa mkaza mwana wa marehemu ambaye ni babake seneta.

Mahakama imeahirisha vikao vyake hadi Jumatano kwa sababu Bi Kitani hakuwepo mahakamani.