Habari Mseto

Kitendawili cha kifo cha mwalimu mwanablogu aliyepatikana amefariki

April 7th, 2024 2 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

POLISI mjini Kisii wameanzisha uchunguzi kuhusu kifo cha mwalimu, ambaye mwili wake ulipatikana ukining’inia kwenye kibanda katika kisa kinachoshukiwa kuwa ni mauaji.

Marehemu, Duke Nyabaro, 32, pia alikuwa mwanablogu, ambaye amekuwa akitoa maoni mengi kuhusu siasa za Kisii, haswa katika eneobunge la Bonchari, anakotoka.

Shingo ya marehemu ilikuwa imefungwa kwa kipande cha kitambaa kwenye kibanda ili kuonekana kana kwamba amejitia kitanzi akiwa amepiga magoti.

Haya yalitokea katika kijiji cha Nyaora Corner, eneobunge la Kitutu Chache Kusini.

Mwili wake uligunduliwa mapema Jumapili asubuhi, Aprili 7, 2024 na waumini ambao walikuwa wakienda kusujudu kisha wakaarifu polisi wa eneo hilo.

Kulingana na jamaa zake, waligundua kuwa jamaa yao hakuwa amelala nyumbani kwake Jumapili asubuhi walipopokea simu kutoka kwa nambari isiyojulikana.

“Tulienda nyumbani kwake lakini hatukumkuta. Tulielekea tulipoambiwa na tumkapata,” Bi Mary Machuki alisema.

Walioona mwili wake walisema kulikuwa na maswali mengi ambayo yalihitaji majibu kuhusu jinsi mwalimu alikufa.

“Tunashuku hapa kuna kitendawili. Iwapo kingekuwa kisa cha kujinyonga, nguo zake zingekuwa zimelowa maji kwani kumenyesha usiku kucha hapa Kisii. Ni unyevunyevu kote. Inakuwaje nguo zake zibaki kavu nje ya kibanda hicho,” James Metobo, mkazi aliuliza.

Katika kundi moja la mitandao ya kijamii, mtumiaji mmoja alimtaja marehemu kuwa mwenye maono na mwalimu wa kupigiwa mfano ambaye aliheshimu kila mtu.

“Hakuwa na mpaka wowote wa kisiasa. Tabia yake ya ujamaa ilimfanya aheshimiwe kote Kaunti ya Kisii,” mtumiaji huyo alisema.

Kamanda wa polisi katika Kaunti ya Kisii Charles Kases alithibitisha kisa hicho.

“Ni kweli kwamba mwili ulipatikana. Tumeanzisha uchunguzi kuhusu kisa hicho. Uchunguzi wa maiti utatusaidia kubaini ikiwa ni mauaji au ni kujiua,” Bw Kases aliambia Taifa Dijitali kwa simu.

Marehemu alikuwa mwalimu katika mojawapo ya shule eneo la Kehancha, Kaunti ya Migori na alikuwa amerejea nyumbani baada ya kufunga kwa likizo ya Aprili.

Mwili wake ulihamishiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii (KTRH).

 

[email protected]