Habari

Kitendawili cha mauaji ya wanawake Nairobi

February 13th, 2019 2 min read

Na WYCLIFFE MUIA

MWILI wa mwanaharakati Caroline Mwatha Ochieng Jumanne ulipatikana katika hifadhi ya maiti ya City, Nairobi, siku saba baada ya mwanaharakati huyo kuripotiwa kutoweka mtaani Dandora, Nairobi.

Maafisa wa polisi wanaochunguza kisa hicho walidokezea Taifa Leo kuwa mwili wa mwanaharakati huyo ulipelekekwa na ‘raia wa kawaida’ kutoka Hospitali ya Kenyatta (KNH), Nairobi.

Rekodi za polisi zinaonyesha kuwa mwili wa Bi Mwatha ulitolewa katika Hospitali ya Kenyatta na mtu aliyejitambulisha kama mumewe.

Maafisa wanaochunguza kesi hiyo wanasema mtu huyo aliyejitambulisha kama mkewe mwanaharakati huyo alipata kibali kutoka kituo cha polisi cha Kenyatta ili kupeleka mwili wake katika hifadhi ya maiti ya City.

Polisi walidai kuwa Bi Mwatha, ambaye ni mama wa watoto wawili, alikuwa na ujauzito wa miezi mitano na alikufa akijaribu kuavya mimba katika kliniki moja jijini Nairobi.

“Mmiliki wa kliniki pamoja na daktari mmoja walijitokeza na kukiri kuwa walipeleka mwili wake katika Mochari ya City na kuandikisha jina lisilo lake na kuripoti kuwa alikufa baada ya kuhara,” afisa wa polisi ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema.

Maafisa wa ujasusi waliambia shirika la AFP kuwa waliona jumbe za simu zilizohusu mpango wa Bi Mwatha wa kuavya mimba.

Msemaji wa Polisi Charles Owino alithibitisha kukamatwa kwa mmiliki huyo wa kliniki na daktari husika.

“Wawili hao ambao ndio waliopeleka maafisa wa ujajusi katika mochari wanaendelea kuzuiliwa na polisi,” alisema Bw Owino.

Uavyaji mimba ni haramu nchini Kenya na sharti kliniki au daktari awe na leseni ya kuavya mimba iwapo maisha ya mama yamo hatarini.

Caroline Mwatha aliyekuwa mwanaharakati wa shirika la Dandora Community Social Justice Centre aliyepatikana ameuawa jana na mwili wake kupelekwa katika mochari ya City, Nairobi. Picha/Hisani

Polisi wanasema mwili wa mwanaharakati huyo ulipelekwa katika mochari ya City Februari 7 lakini familia ilisema haikupata mwili wake siku hiyo hiyo ilipokuwa inatafuta mwili wake eneo hilo.

Baadhi ya jamaa zake walisema mwili wa Bi Mwatha haukuwa na majeraha yoyote lakini wakapinga madai ya polisi kuwa aliaga akiavya mimba.

Mashirika ya kijamii yalikuwa yameanza maandamano kushinikiza polisi wamtafute Bi Mwatha hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa mwanaharakati aliyepinga mauaji ya polisi ya kiholela kupitia shirika la Dandora Community Social Justice Center .

Kifo cha Bi Mwatha kinajiri siku chache baada ya vifo vingine viwili vya Mildred Odira na Mary Wambui vilivyowaacha Wakenya wengi na maswali.

Bi Odira, ambaye alikuwa mtaalamu wa simu katika kampuni ya habari ya Nation Media Group (NMG) alitekwa nyara katika hali tatanishi, ambapo mwili wake ulipatikana baadaye katika mochari ya City, Nairobi baada ya kutafutwa kwa zaidi ya wiki moja na familia yake.

Kilichoibuka baada ya upasuaji wa mwili huo ni kwamba aliuawa kinyama -kabla ya kutupwa barabarani na kukanyagwa na magari.

Naye Wambui ambaye mwili wake ulipatikana eneo la Ruiru anadaiwa kuuawa katika nyumba ya mpenzi wa mumewe eneo la Kiambu kabla ya mwili wake kusafirishwa kwenda kutupwa.

Mwezi uliopita, mwanafunzi Carilton Maina alipatikana ameuawa kitatili katika mtaa wa Kibera jijini Nairobi, ambapo mwili wake ulikuwa na majeraha ya risasi.

Ripoti zilisema mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza, aliuawa na polisi kwa kutuhumiwa kuwa miongoni mwa kundi la vijana waliokuwa wakiwahangaisha wakazi.

Mnamo 2016 wakili Willie Kimani na mteja wake pamoja na dereva wa teksi walipatikana wameuwa kinyama na miili yao kutupwa mtoni.