Habari Mseto

Kitendawili cha mwanamke aliyepatwa ameuawa muda mfupi baada ya kuonekana baa

June 4th, 2024 1 min read

NA GEORGE MUNENE

MWANAMKE mmoja alipatikana Jumatatu ameuawa na mwili wake kutupwa katika mtaro wa kuelekeza maji katika shamba la mpango wa kilimo cha unyunyiziaji katika kijiji cha Kamuchege, Kaunti ya Kirinyaga.

Mwili wa mwendazake ulipatikana bila nguo ishara kwamba huenda alibakwa kabla ya kuuawa kikatili. Wanakijiji walipata mwili wa marehemu, mwenye umri wa miaka 37, walipokuwa wakielekea katika mashamba yao na ndipo wakapiga ripoti katika Kituo cha Polisi cha Wang’uru.

“Tulipata mwili huo mwendo wa asubuhi na kuwapasha habari maafisa wa polisi. Kinachoshangaza ni kwamba mwanamke huyo hakuwa na mavazi,” mwanakijiji mmoja, Mary Wangui, akasema.

Wakazi sasa wanataka kisa hicho kichunguzwe na wale waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria.

“Kwa nini umvue nguo mwanamke na kumuua?” akauliza Bw Joseph Muchiri.

Wapelelezi wanasema mwendazake ambaye anatoka eneo la Gitaraka, Embu na alikuwa amemtembelea wifi yake mjini Kirinyaga wakati alipokumbana na mauti.

Kabla ya mauti yake, mwanamke huyo alikuwa ameonekana kwenye baa moja mjini akinywa vileo lakini hakurudi nyumbani kwa wifi yake.

Polisi wanaamini kwamba mwendazake alinyongwa hadi akafa kwa sababu shingo yake ilikuwa imefura.

Mkuu wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Mwea Mashariki Patrick Nyaanga alisema uchunguzi umeanzishwa kubaini kilichosababisha mauaji ya mwanamke huyo mchanga.

Aliwataka wenyeji kusaidia kutambua washukiwa ili waadhibiwe kwa kosa hilo la kinyama.