Habari Mseto

Kitendawili kuhusu michoro ya graffiti kwenye matatu kama alivyoagiza Uhuru

November 13th, 2018 1 min read

Na LEONARD ONYANGO

MATATU zilizo na michoro mbalimbali almaarufu Graffiti huenda zikajipata matatani baada ya serikali kuanza kutekeleza tena sheria za usalama wa barabarani Jumatatu.

Inspekta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet wiki iliyopita aliagiza wamiliki wa matatu kuondoa michoro hiyo kufikia Jumatatu (jana) kulingana na matakwa ya Sheria za Michuki.

Agizo hilo la Inspekta Jenerali Boinnet linakinzana na agizo lililotolewa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2014 ambapo alisitisha sheria hiyo na akawataka wamiliki wa matatu kuendelea kuchora katika magari ya umma kutokana na kigezo kwamba michoro hiyo inatoa nafasi ya ajira kwa vijana.

Rais Kenyatta alisema michoro hiyo inawezesha vijana kutumia vipaji vyao kujikimu kimaisha. Agizo la Bw Boinnet limepingwa vikali na wadau katika sekta ya umma. Mwenyekiti wa Chama cha Wahudumu wa Matatu katikati ya Jiji la Nairobi Jamal Ibrahim ameshikilia kuwa polisi hawana mamlaka ya kufutilia mbali agizo la Rais.

Kulingana na Bw Ibrahim, michoro hiyo katika matatu haichangii kwa vyovyote vile katika kutokea kwa ajali.

Lakini Bw Boinnet amesisitiza kuwa ni sharti Sheria za Michuki zifuatwe kikamilifu.Inspekta Jenerali alisema michoro inayokubalika ni ile inayoenzi mashujaa wa humu nchini kama vile wanariadha.

Huku baadhi ya watu wakilalama kuwa kupigwa marufuku kwa michoro katika mabasi ni kunyima vijana fursa ya kutumia vipawa vyao katika uchoraji kujipa mapato, baadhi ya wataalamu pia wanakiri kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuleta nidhamu katika usafiri wa umma.

Wanaounga mkono marufuku hiyo wanasema kuwepo kwa mpangilio katika mwonekano wa matatu ni hatua muhimu katika kudumisha nidhamu.

Wasanii wa uchoraji hujipatia kati ya Sh50,000 na Sh100,000 kuchora basi lenye uwezo wa kubeba abiria 33 na kati ya Sh10,000 na Sh20,000 gari la viti 14.

Sheria za Michuki zinapiga marufuku michoro na uchezaji wa muziki kwa sauti ya juu ndani ya matatu.