Kituo cha Covid-19 kimeundwa Pumwani – Amoth

Kituo cha Covid-19 kimeundwa Pumwani – Amoth

Na CHARLES WASONGA

KAIMU Mkurugenzi wa Afya Patrick Amoth amesema kituo cha kuwatenga wagonjwa wa Covid-19 kimebuniwa katika Hospitali ya kujifungulia akina mama ya Pumwani.

Akiongea Jumanne baada ya kuzuru hospitali hiyo Dkt Amoth amesema vyumba hivyo vilivyoko katika Chuo cha Uuguzi vitawahudumia wahudumu wa afya katika hospitali hiyo pekee na wafanyakazi wengineo.

Hii ni kufuatia tukio ambapo wafanyakazi 41 wa hospitali hiyo walithibitishwa kuwa na virusi vya corona.

“Tumeafikiana kuwa kuanzia leo Jumanne, tutakuwa na eneo maalum, katika Chuo cha Uuguzi, ya kuwatenga wafanyakazi walioambukizwa,” amesema Dkt Amoth.

Wafanyakazi 22 miongoni mwa waliopatikana na virusi, akasema, ni wale wa madaraja ya chini.

Dkt Amoth alisema visa hivyo vilithibitishwa baada sampuli kutoka kwa wafanyakazi wote 290 kuchunguzwa.

Alisema wale wote walioambukizwa Covid-19 hawana magonjwa mengine, na hivyo hamna hofu ya hali yao kuwa mbaya zaidi.

Wafanyakazi walioambukizwa ni maafisa wawili wa matibabu, maafisa wa kliniki (2), wauguzi (14) na mtaalamu mmoja wa maabara.

Wauguzi wawili wanaohudumu katika kitengo cha watoto wachanga na watatu wanaohudumu katika chumba cha upasuaji, na mwingine anayefanya kazi katika wadi ya wanawake wajawazito, ni miongoni mwa wale ambao watatengwa nyumbani.

Usimamizi wa Hospitali hiyo ulisema hakuna watoto wachanga waliambukizwa corona japo akina mama wawili walipata ugonjwa huo miezi miwili iliyopita.

Mkurugenzi wa Afya katika Idara ya Huduma za Nairobi Josephine Kibaru alisema japo hospitali hiyo haijafungwa, imepunguza shughuli zake.

“Kutokana na uhaba wa wafanyakazi, baada ya wengi wao kujitenga, vituo vingine vya afya kama vile Ngara na Eastleigh vitatumika na akina mama kujifungua,” akasema.

You can share this post!

COVID-19: Visa vipya 497 vyathibitishwa idadi jumla...

Mbunge akiri walimu wa shule za wamiliki binafsi wanapitia...

adminleo