Habari

Kituo cha polisi cha Githurai Mwiki chazinduliwa rasmi

July 3rd, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

HALI ya usalama na huduma za polisi kwa umma eneo la Githurai inatarajiwa kuimarika baada ya kituo cha Polisi cha Githurai 45, Mwiki kilichoko katika eneobunge la Ruiru, Kiambu na kiungani mwa jiji la Nairobi kuzinduliwa rasmi.

Mnamo Alhamisi, katika hafla iliyoongozwa na Naibu Inspekta Mkuu wa Polisi (DIG) Edward Mbugua, kituo hicho kilipata afisi ya msimamizi wa kituo cha polisi.

Aidha, kitengo cha upelelezi wa jinai (DCI) pia kilizinduliwa pamoja na seli.

Kabla Rais Uhuru Kenyatta 2018 kutangaza mikakati kuimarisha idara ya polisi, hatua iliyopelekea kikosi cha maafisa wa kawaida na baadhi ya wa kikosi tawala (AP) kujumuishwa kuunda kikosi maalum NPS, kituo hicho kilikuwa chini ya maafisa wa AP, na kilichosimamiwa na afisa aliye na ngazi ya Inspekta.

Kufuatia sura mpya iliyozinduliwa, DIG Mbugua alisema kiwango cha maafisa kitaongezwa zaidi ili kuimarisha utendakazi kwa umma.

“Nimeagiza kamanda msimamizi wa kaunti (Kianbu) kuongeza maafisa 20 zaidi. Kwa sasa tuna maafisa 20 pekee na kufikia wiki ijayo tutakuwa tumepokea wengine zaidi,” Bw Mbugua akasema.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na mbunge wa Ruiru Simon King’ara.

Uimarishaji wa kituo hicho ulifadhiliwa kupitia fedha za hazina ya ustawi wa maeneobunge (NG-CDF) Ruiru.

Akiridhia hatua hiyo ya maendeleo, Bw King’ara alieleza imani yake kuwa hali ya usalama eneo la Githurai itaimarika.

“Tumekuwa tukitegemea kituo cha polisi cha Ruiru Mjini na Kimbo, leo tunashukuru kupata kingine. Ujenzi na uimarishaji umefadhiliwa kupitia NG-CDF,” mbunge huyo akaambia wanahabari.

Bw King’ara pia alisema kituo hicho kitapata gari rasmi kufanikisha utendakazi kwa umma.

Mbunge huyo pia alifichua kwamba eneo la Mwihoko na Gatongora, yote yaliyoko katika eneobunge la Ruiru yatapata vituo vipya vya polisi ili kusaidia kuimarisha hali ya usalama.

Mbunge wa Ruiru Simon King’ara akipanda mti baada ya kuzindua kituo cha polisi cha Githurai 45 Mwiki. Picha/ Sammy Waweru

Kituo hicho kimezinduliwa huku Inspekta Muu wa Polisi (IG) Hillary Mutyambai akiahidi vituo vingi vya polisi nchini kujengwa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

DIG Mbugua alipongeza maafisa wa polisi wa Githurai 45 Mwiki kwa kile alitaja kama kusaidia kutekeleza sheria na mikakati iliyowekwa kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.

Alisema Githurai, ikilinganishwa na mitaa mingine Nairobi na viungani mwa jiji la Nairobi imeandikisha visa vichache vya maambukizi ya ugonjwa huu unaosababishwa na virusi vya corona.

“Ninawapongeza na kuwashukuru kwa utendakazi wenu bora,” Bw Mbugua akaambia maafisa wa kituo hicho.

Hafla ya kuzindua kituo hicho pia ilidhuhuriwa na maafisa wakuu wa polisi kaunti ya Kiambu na Nairobi, na diwani wa wadi ya Mwiki Githurai James Kimani Mburu (Kidim).