Kituo cha polisi kujengwa eneo la Gatong’ora

Kituo cha polisi kujengwa eneo la Gatong’ora

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Gatong’ora kilichoko mjini Ruiru, wamepata afueni baada ya serikali kutenga fedha za kujenga kituo cha polisi.

Kwa muda mrefu hali ya usalama ilikuwa imezorota huku kila mara watu wakipoteza maisha yao.

Ni baada ya wakazi wa kijiji hicho kulalamika kwa muda mrefu ndipo serikali kuu ilitenga takribani Sh50 milioni ya kujenga kituo cha polisi eneo hilo.

Mbunge wa Ruiru, Bw Simon King’ara, alisema kwa muda mrefu hali ya usalama imezorota na kwa hivyo mradi wa kujenga kituo cha polisi una umuhimu.

“Wakazi wengi wamekuwa wakilalamika kuhusu usalama uliozoroteka na kwa hivyo serikali imechukua jukumu la kujenga kituo hicho,” alisema Bw King’ara.

Alisema hivi majuzi kituo cha Mwiki eneo la Githurai kilifunguliwa kuanza kuwafaa wakazi wa eneo hilo.

Kuna mpango wa serikali kujenga kituo kingine eneo la Mwihoko, Ruiru ili kukabiliana na hali mbaya ya usalama.

Mkazi Bw Anthony Mbugua wa kijiji cha Gatong’ora anasema kwa muda mrefu wahudumu wa bodaboda ndio wameathirika pakubwa.

 

Mradi huo wa kujenga kituo cha polisi tayari umeanza ambapo afisi ya chifu na ukumbi wa mapumziko kwa wananchi pia utajumuishwa kwenye ujenzi huo.

Wakazi wa eneo hilo walisema kuwa siku chache zilizopita mlinzi mmoja wa usiku aliuawa na wahuni alipokuwa kazini.

Kulingana na Bw Mbugua, kijiji cha Gatong’ora kina idadi kubwa ya wakazi na huwa wanatembea kilomita nne hadi mjini Ruiru kuripoti matukio ya uhalifu.

Mji wa Ruiru una idadi kubwa ya watu ambao ni zaidi ya 200,000 na ni hali iliyochngiwa pakubwa na neema za barabara ya Thika Superhighway.

You can share this post!

Rionoripo na Kiptanui kuongoza Wakenya 8 Berlin Marathon

HASLA BANDIA