Kituo cha uchinjaji na utayarishaji wa nyama ya kuku kujengwa Nairobi

Kituo cha uchinjaji na utayarishaji wa nyama ya kuku kujengwa Nairobi

NA SAMMY WAWERU

SERIKALI ya Kaunti ya Nairobi imesema itajenga kituo cha kuchinjia kuku ili kuafikia ubora kiafya wa nyama jijini.

Idara ya vetinari Nairobi, imedokeza tayari fedha za mradi huo zimetengwa kupitia makadirio ya bajeti mwaka wa fedha 2022/2023.

Ujenzi wa buchari hiyo unatarajiwa kuanza baadaye mwaka huu, au mwanzoni mwa mwaka ujao, 2023.

Kituo hicho aidha kinapangiwa kukamilika mwishoni mwa 2023 au mwaka wa 2024 ukianza.

“Kaunti ya Nairobi haina buchari maalum iliyoidhinishwa kutekeleza uchinjaji wa kuku. Katika makadirio ya bajeti mwaka wa fedha 2022/2023, tumetenga mgao kujenga kituo maalum,” Dkt Muriuki Kabatha, Naibu Mkurugenzi Idara ya Vetinari Nairobi akaambia Taifa Leo, kupitia mahojiano ya kipekee.

Buchari hiyo ya kuku itajengwa katika kaunti ndogo ya Kasarani, na imebajetiwa kugharimu Sh8 milioni.

Kuku wa mfugaji kiungani mwa jiji la Nairobi. Serikali ya kaunti ya Nairobi inapanga kujenga kituo cha kuchinjia kuku. PICHA | SAMMY WAWERU

Msukumo wa mradi huo unatokana na kuendelea kuongezeka kwa idadi ya wafugaji wa kuku jijini Nairobi.

Nairobi inakadiriwa kuwa na zaidi ya wafugaji 400 wa kuku.

Kufuatia uhaba wa ardhi na changamoto za mazingira – majaa ya taka, wataalamu wa mifugo wanaonya utupaji kiholela wa viungo vya kuku au kuku waliofariki ni hatari na unaweza kuchangia mkurupuko wa magonjwa hatari ya wanyama kwa binadamu.

“Magonjwa kama vile Salmonella yanatokana na mazingira machafu ya kuku, na ni hatari kwa binadamu,” aonya Dkt Victor Yamo, Meneja wa Uhamasishaji Kampeni Haki za Mifugo, katika Shirika la World Animal Protection.

Kaunti ya Nairobi ina vichinjio vitatu vilivyoko Kariokor, Burma Market na Burma Maziwa, ambavyo kulingana na Dkt Kabatha havijaafikia vigezo vinavyohitajika.

Kulingana na afisa huyo, mpango wa ujenzi wa kituo cha kisasa utashirikisha wawekezaji wa kibinafsi.

“Serikali ya kaunti itatoa nafasi ya ardhi,” akasema.

Kufuatia upungufu wa ardhi na mashamba kutokana na ongezeko la idadi ya watu, wengi wamekumbatia ufugaji wa kuku.

Nyama ya kuku ni miongoni mwa zenye walaji wengi.

  • Tags

You can share this post!

Rais Kenyetta amsimamisha kazi Jaji Chitembwe

GWIJI WA WIKI: Were Mukhusia

T L