Habari Mseto

Kituo cha utafiti kufunguliwa MKU

December 9th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kimepitisha mpango wa kubuni kituo cha utafitii kwa lengo la kujiendeleza zaidi masomoni, amesema Prof David Serem.

Alisema Ijumaa wiki jana kwamba kutakuwa na sehemu mbili katika mpango huo; nazo ni kwa wanafunzi wanaoendeleza masomo yao cha kiwango cha juu na wale wa utafiti.

“Mpango huo ni wa miaka mitano ili kuona jinsi utakavyoboresha maswala ya elimu ya juu. Chuo cha Mount Kenya kinafanya juu chini kuona ya kwamba mpango huo unafana,” alisema Prof Serem.

Aliyasema hayo wakati wa kufuzu kwa wahitimu wapatao 5,000 wa MKU.

Aidha, alisema chuo hicho kinafanya juhudi kuona ya kwamba kinaboresha maswala ya afya, mapishi,na usalama katika mazingira yake.

Prof Serem alisema MKU ina mpango wa kuwakatia bima ya afya wafanyakazi wake wote kuanzia mwaka ujao wa 2020.

“Bima hiyo inasimamia ajali, kifo, na kupata jeraha lolote kwa mfanyakazi wa chuo hiki. Hii ni njia moja ya kujali masilahi ya wafanyakazi wetu hapa chuoni,” alisema Prof Serem.

Alisema maswala hayo yote ni muhimu kwa mwanafunzi yeyote aliye katika chuo hicho.

Wakati wa hafla hiyo chuo hicho kilishuhudia kupata naibu chansela mpya; Prof Peter Wanderi ambaye amechukua nafasi ya Prof Stanely Waudo ambaye aliendesha chuo hicho kwa zaidi ya miaka 10.

Chansela wa chuo hicho Prof John Struthers alisema tayari chuo hicho kimeweka mkataba wa pamoja na Chuo cha Manchester Metropolitan, Uingereza ambapo mkataba huo ulitiwa sahihi mwezi Septemba.

Alisema wanafunzi wa pande zote mbili watapata nafasi ya kubadilishana mawazo na kutembeleana katika vyuo vyote viwili.

Alisema chuo hicho kitawafadhili wanafunzi wanaoendesha masomo ya juu ya uuguzi huku akisema ni njia moja ya kupata maafisa wa afya walio na ujuzi kamili kuhusu masuala ya afya.