Kituo cha Walibora hatarini kufifia baada ya kifo chake

Kituo cha Walibora hatarini kufifia baada ya kifo chake

GERALD BWISA na ELVIS ONDIEKI

KITUO cha kusambazia watoto vitabu kilichoanzishwa na msomi mashuhuri wa Kiswahili, marehemu Prof Ken Walibora, kinakumbwa na changamoto tele baada ya kifo chake.

Prof Walibora alianzisha kituo hicho cha Ken Walibora Centre for Literature Development katika mwaka wa 2019, akiwa na lengo la kuwawezesha wanafunzi kusoma vitabu 400 vya hadithi kabla ya kukamilisha Kidato cha Nne.

Kituo hicho kinachopatikana katika orofa ya saba ya jengo la Purshottam Place, barabara ya Westlands jijini Nairobi, kingali kimefunguliwa kwa ufadhili wa familia yake iliyo Amerika.

Mbali na kifo chake kilichotokea Aprili 10, 2020, changamoto zinazokumba kituo hicho zimesababishwa na jinsi ratiba ya shule ilivyovurugika na vilevile matatizo yanayotokana na janga la corona.Kulingana na mratibu wa kituo hicho, Bw Paul Watila, kituo hicho kilianzishwa ili wanafunzi wasome bila vikwazo wanavyopata wakati wanaposoma kwa minajili ya mitihani shuleni.

Mwanafunzi huhitajika kujisajili na Sh1,200 kwa mwaka, iliyo sawa na Sh100 kwa mwezi, ambapo anaruhusiwa kupata vitabu vine kila mwezi: Viwili vya Kiswahili na viwili vya Kiingereza.

“Aliamini wanafunzi hawafai kununua vitabu. Vitabu vilikuwepo. Angevinunua na kuviweka katika kituo hiki. Ada waliyolipa wanafunzi ilinuiwa tu kuwafanya wawajibike,” akasema.

“Mwaka uliopita tulipompoteza Prof Walibora, tulikuwa na zaidi ya wanafunzi 1,000 waliosajiliwa. Sasa tuna zaidi ya wanafunzi 2,000 waliosajiliwa. Huwa wanapata vitabu hivi hata wanapokuwa nyumbani,” akaongeza.

Kituo hicho ni mojawapo ya sifa kuu alizoacha Walibora ambazo zilitajwa wakati wa hafla ya kumbukumbu yake iliyoandaliwa Jumamosi iliyopita.Hafla hiyo iliyofanyika kwa zaidi ya saa sita kupitia mtandaoni, ilihudhuriwa na wasomi wengi wa Kiswahili.

Mjane wa Prof Walibora, Ann, pia alihudhuria na kushukuru kwa juhudi zinazoendelezwa kumkumbuka mume wake.Mwaka mmoja baada ya Prof Walibora kufariki katika ajali ya barabarani Nairobi, kuna mengi yanayoendelea kufichuka kuhusu maisha ya mwandishi huyo mashuhuri aliyepata umaarufu kwa kuandika vitabu kama vile Siku Njema na Kidagaa Kimemwozea.

Kakake, Bw Patrick Wafula aliambia Taifa Leo kuwa Walibora alikuwa msiri sana, na wanapata changamoto kutambua mali alizomiliki.

“Hakutuambia kila kitu wakati alipokuwa hai,” akasema Bw Wafula, ambaye aliongeza kuwa wanatarajia mashirika ya serika yatasaidia familia yake kutambua mali zake zote.

You can share this post!

Afisa adai aliadhibiwa kwa kutopelekea Ruto umati

Shirika linavyohangaishwa na wanyakuzi wa ardhi