Makala

KIU YA UFANISI: Mradi wa maziwa unaonawiri na kunufaisha 1,300

September 26th, 2019 2 min read

Na PHYLLIS MUSASIA

FAMILIA 25 za wafugaji ng’ombe wa maziwa katika eneo la Subukia, Kaunti ya Nakuru, zina kila sababu ya kutabasamu baada ya kampuni ya maziwa ambayo imekuwepo kwa kipindi cha miaka 12 sasa kuonekana kunawiri.

Kampuni hiyo kwa jina ‘Suka Cooperative Society’ ndio ya pekee eneo hilo baada ya kampuni zinginezo kudidimia.

Kulingana na David Kangethe ambaye ni mwenyekiti wa kampuni hiyo, msukumo mkubwa uliopekelea familia hizo kuungana na kuanzisha mradi huo ambao sasa unahudumia wakulima zaidi ya 1,000 ulitokana na bei duni ya maziwa waliyoshuhudia kutoka kwa madalali

Kangethe alieleza kuwa wakulima wengi walitatizika kiuchumi kutokana na hali hiyo ambayo walilazimika kuuza lita ya maziwa kwa Sh8 pekee.

“Hali ilikuwa mbaya na wengi wetu walizidi kukadiria hasara hata baada ya kufanya bidii na kuhakikisha kuwa ng’ombe wetu wanatoa maziwa mengi na yenye ubora na uzito ufaao,” akasema.

Kulingana naye, mwanzoni familia hizo zilikuwa na ugumu wa kusajili kampuni hiyo hata baada ya kuelewana kuwa kila mmoja atoe Sh500.

“Baada ya kukusanya pesa hizo, tuligundua kuwa zilikuwa chini ya kiwango ambacho kilihitajika na ikatubidi tuongeze kiwango cha mchango wa kila mmoja hadi Sh2,000,” akaongeza mwenyekiti huyo.

Baada ya kuisajili kampuni ya Suka mwaka wa 2009, wakulima hao walijitosa katika harakati za kutafuta soko la maziwa ya kampuni yao.

“Haikuwa rahisi hata baada ya kukamilisha usajili na bodi husika. Tulijituma kwa sana kuhakikisha kuwa tunapata soko la maziwa yetu baada ya kupitia katika mchakato kamili,” akasema Nancy Waithera ambaye ni mmoja wa wanachama.

Mnamo mwaka wa 2015, wanachama wa kampuni hiyo walipata mafunzo kutoka kwa wataalamu wa idara ya kilimo na mifugo na kusaidika sana kuhusu jinsi ya kupokea maziwa kutoka kwa wakulima, kuyatengeza na kisha kuhifadhi inavyotakikana.

“Kampuni hii ina jumla ya wanachama 1, 300 na wao ndio hutuletea maziwa. Kwa siku moja tunapokea zaidi ya lita 47,000 na kwa kila lita tunanunua kwa Sh37,” akaeleza Kangethe.

Alisema kuwa wakati wa kuuza, kampuni ya Suka huuza lita moja kwa Sh50 wakati wa msimu wa kawaida na wakati wa kiangazi bei hiyo hupanda hadi Sh54.

Aidha, kampuni hiyo ina uwezo wa kuhifadhi hadi lita 62,000 za maziwa kila siku.

Suka, ambayo iko kwenye mpaka wa kaunti za Nakuru na Nyandarua, imeweza kuvutia idadi kubwa ya wawekezaji ambao wamefurahishwa na jinsi vile wanazidi kunawiri.

Kangethe alieleza kuwa baadhi ya changamoto ambazo kampuni hiyo inapitia ni pamoja na soko la ushindani mkali ikizingatiwa kuwa maeneo ya Nakuru na Nyandarua yanajulikana kwa uwezo mkubwa wa wakulima wa maziwa.

Kupoteza wanachama

Changamoto nyingine alisema ni kupoteza wanachama ambao hupoteza hamu kwenye shughuli za kampuni haswa kwa sababu wako na kiwango cha chini cha mgao wa kampuni, mbinu mbovu za siasa na pia mabadiliko ya bei ya bidhaa kila wakati.

Mnamo Julai, kampuni hiyo ilianzisha mradi wa kutengezea bidhaa nyingine kama vile ‘yoghurt’ na maziwa mala.

Kangethe alisema kuwa mradi huo mpya umesaidia sana kampuni ya Suka kuongeza mapato yake.

“Licha ya kuwasaidia mamia ya wakulima wa hapa na Nyandarua, tuko pia kwenye biashara. Tunafanya bidii kuona kuwa wakulima wanapoendelea kiuchumi kampuni pia inazidi kuua,” akasema.

Wakulima waliotoa maoni yao kuhusu kampuni ya Suka walisema kuwa wanapokea malipo yao kwa wakati ufaao na kwamba hawajaweza kupata matatizio yoyote kutokana na usimamizi wake.

Rosaline Cherotich alisema amekuwa mwanachama tangu kampuni hiyo ilipoanza na kwamba ameweza kuwalipia wanawe karo na pia kuhakikisha kuwa ng’ombe wake wanapata lishe na dawa bila kutatizika.

“Maziwa ninayouza kwenye kampuni ya Suka ndio huwalipia wanangu karo. Chakula tunachokula nyumbani kando na kile ambacho tunapata shambani mwetu, sisi hununua kutoka kwa pesa za maziwa,” akasema Cherotich aliyepeleka lita 20 za maziwa kiwandani kila siku.