Michezo

Kiungo Michael Cuisance atua Marseille baada ya uhamisho wake hadi Leeds United kugonga mwamba

October 6th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KIUNGO Michael Cuisance, 21, amejiunga na Olympique Marseille kwa mkopo wa mwaka mmoja kutoka Bayern Munich.

Uhamisho huo ulirasimishwa siku tatu baada ya juhudi za Leeds United kujitwalia huduma za nyota huyo raia wa Ufaransa kugonga ukuta.

Cuisance alikuwa pua na mdomo kuingia katika sajili rasmi ya Leeds United wanaonolewa na kocha Marcelo Bielsa kwa kima cha Sh2.8 bilioni kabla ya mpango huo kutibuka kufuatia madai kwamba alipatikana na jeraha wakati akifanyiwa vipimo vya afya.

Marseille kwa sasa watakuwa huru kumpa Cuisance mkataba wa kudumu mwishoni mwa kipindi chake cha mkopo kambini mwao.

Cuisance alichezeshwa na Bayern Munich katika jumla ya mechi 10 katika msimu wa 2019-20 na akawafungia bao moja. Alitokea benchi katika kipindi cha pili katika ushindi wa 8-0 uliosajiliwa na Bayern dhidi ya Schalke katika mechi ya kwanza ya Bundesliga msimu huu.

Chipukizi huyo alihamia Bayern mnamo Agosti 2019 baada ya kushawishiwa kuagana na Borussia Monchengladbach ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa kima cha Sh1.4 bilioni.

Cuisance alikuwa mchezaji wa akiba ambaye hakutumiwa katika gozi la Uefa Super Cup lililowakutanisha Bayern na Sevilla mnamo Septemba 24, 2020. Hata hivyo, aliachwa nje ya kikosi kilichotegemewa na kocha Hansi Flick katika mechi ya Bundesliga iliyoshuhudia Bayern wakipokezwa kichapo cha 4-1 kutoka kwa Hoffenheim mnamo Septemba 27, 2020.

Cuisance alisalia benchi katika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) iliyoshuhudia Bayern wakizamisha chombo cha Paris Saint-Germain (PSG) kwa bao 1-0 jijini Lisbon, Ureno mnamo Agosti 23, 2020.

Iwapo uhamisho wake hadi Leeds United ungalifaulu, basi angalikuwa mchezaji wa tano kusajiliwa na kocha Bielsa ambaye tayari alijitwalia maarifa ya Rodrigo Moreno (Sh3.6 bilioni) kutoka Valencia, Diego Llorente (Sh2.5 bilioni) kutoka Real Sociedad, Robin Koch (Sh1.8 bilioni) kutoka Freiburg na aliyekuwa fowadi wa zamani wa Wolves, Helder Costa (Sh2.2 bilioni).