Kiungo Mkenya-Mwingereza Henry Ochieng’ atangaza kugura mabingwa wa zamani wa Ireland Cork City

Kiungo Mkenya-Mwingereza Henry Ochieng’ atangaza kugura mabingwa wa zamani wa Ireland Cork City

Na GEOFFREY ANENE

KIUNGO wa kimataifa wa Kenya, Henry Ochieng’ ameondoka Cork City FC baada ya kampeni ya kusikitisha katika klabu hiyo kutoka Jamhuri ya Ireland iliyoangukiwa na shoka kwa kuvuta mkia kwenye Ligi Kuu msimu uliopita.

Mzawa huyo wa jiji la London, ambaye alijiunga na Cork City mnamo Januari 31, 2020 kutoka Wingate FC, alikuwa mmoja wa wachezaji waliojituma zaidi msimu uliopita.

Alitangaza kuondoka kwake Januari 25, 2021 kupitia mtandao wake wa Twitter.

“Shukran kila mtu @CorkCityFC kwa msimu mmoja nilikuwa hapo. Nilikutana na watu wazuri na ninashukuru kuchezea klabu ya kifahari kama hiyo. Nawatakia kila la kheri kwa miaka ijayo,” alisema. Cork City ilijibu ujumbe wake kwa kusema, “Tunakutakia mema, Henry!”

Ochieng’, 22, hajawakilisha Kenya kimataifa, lakini aliwahi kujumuishwa katika kikosi cha mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) 2019 dhidi ya Sierra Leone iliyofaa kusakatwa jijini Nairobi mwezi Novemba 2018. Mchuano huo ulifutiliwa mbali baada ya Sierra Leone kupigwa marufuku na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) wiki chache kabla ufanyike kutokana na serikali kuingilia masuala ya shirikisho la soka nchini humo.

Kabla ya kuwa Cork City, Ochieng’ alichezea timu za chipukizi za West Ham U18 na Leyton U18, akaingia timu ya watu wazima ya Leyton Orient na kisha kuhamia Braintree, Welwyn Garden City na Wingate zote nchini Uingereza. Hajatangaza anaelekea wapi baada ya kuondoka Cork City ambayo aliichezea mechi 19 katika mashindano yote msimu uliopita.

  • Tags

You can share this post!

Kanisa la Glory OutReach Assembly lazingatia kuhubiri amani

Felix na Suarez waibeba Atletico dhidi ya Valencia ligini