Kiungo na nahodha wa Ghana, Andre Ayew, kuagana na Swansea City mwisho wa Juni 2021

Kiungo na nahodha wa Ghana, Andre Ayew, kuagana na Swansea City mwisho wa Juni 2021

Na MASHIRIKA

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

KIUNGO mvamizi Andre Ayew, 31, ataagana na Swansea City mwishoni mwa Juni 2021 baada ya mkataba wake uwanjani Liberty kutamatika rasmi.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ghana amefungia Swansea mabao 35 kutokana na mechi 106 tangu ajiunge upya na kikosi hicho kutoka West Ham United kwa kima cha Sh2.5 bilioni mnamo Januari 2018.

Akiwa mchezaji anayedumishwa kwa mshahara wa juu zaidi kambini mwa Swansea, kuondoka kwa Ayew ni jambo lililotarajiwa baada ya kikosi hicho kushindwa kufuzu kwa soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mwishoni mwa kampeni za msimu wa 2020-21.

Fowadi vetereani Wayne Routledge, 36, amepokezwa mkataba mpya na Swansea na ndiye mwanasoka anayejivunia rekodi ya kuhudumu kambini mwa kikosi hicho kwa kipindi kirefu zaidi baada ya kuwajibishwa zaidi ya mara 300 tangu 2011.

Routledge alipata jeraha baya la goti wakati wa mechi ya mchujo wa kufuzu kwa soka ya EPL dhidi ya Barnsley mnamo Mei 22, 2021.

Ayew alijiunga na Swansea bila ada yoyote kutoka Olympique Marseille ya Ufaransa mnamo 2015. Alisajiliwa na West Ham United kwa kima cha Sh2.8 bilioni baada ya kufungia Swansea mabao 12 kutokana na mechi 35 mnamo 2015-16.

Alirejea Swansea miezi 18 baadaye ila akashindwa kusaidia kikosi hicho kutoteremshwa ngazi kwenye EPL.

Ayew alitumwa Fenerbahce ya Uturuki kwa mkopo msimu uliofuata kabla ya kurejea ugani Liberty mnamo 2019 na amekamilisha kampeni za misimu miwili iliyopita chini ya kocha Steve Cooper akiwa mfungaji bora wa Swansea.

Mchuano wake wa mwisho kambini mwa Swansea ni fainali ya mchujo wa kufuzu kwa EPL 2021-22 iliyowakutanisha na Brentford uwanjani Wembley, Uingereza mnamo Mei 29, 2021.

Ayew angepokezwa mkataba mpya wa miaka miwili iwapo Swansea wangeshinda mechi hiyo iliyowashuhudia wakipepetwa 2-0 ugani Liberty.

Mbali na Ayew, Swansea wanatarajiwa pia kuagana rasmi na mwanasoka Barrie McKay ambaye amehudumu kambini mwa Morecambe kwa miezi 18 iliyopita kwa mkopo.

Wanasoka wengine watakaokatiza uhusiano na Swansea muhula huu ni Declan John, Kieron Freeman, Jordi Govea, Freddie Woodman, Marc Guehi na Conor Hourihane.

Kocha Cooper ambaye ana mwaka mmoja pekee kwenye mkataba wake wa sasa na Swansea anahusishwa pakubwa na mikoba ya Crystal Palace wanamtafuta mkufunzi atakayemrithi Roy Hodgson aliyebanduka ugani Selhurst Park mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kenya Lionesses haijapata mwangaza kutoka Wizara ya Michezo...

Tuwei: Sifan ameweka rekodi ya dunia ya mbio za mita...