Kiungo wa Bandari asifiwa na Adebayor

Kiungo wa Bandari asifiwa na Adebayor

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

KIUNGO mshambuliaji wa Bandari FC na timu ya taifa ya Harambee Stars, Abdalla Hassan amepongezwa kutokana na alivyocheza vizuri kwenye mechi dhidi ya Togo na kati ya aliyevutiwa na mchezo wake ni straika wa zamani wa Arsenal, Emmanuel Adebayor.

Hassan aliweza kufunga mabao mawili kwenye mechi mbili za Harambee Stars, akifunga bao la kusawazisha dhidi ya Misri na akafunga bao lingine wakati Stars ilipoishinda Togo kwa mabao 2-1 na ndipo Adebayor alipomtupia sifa mwanasoka huyo.

Inaaminika Hassan alipewa sifa nyingi na Adebayor anayesemekana alifika katika chumba cha kubadilisha mavazi cha Harambee Stars huko Lome na kuwapongeza wachezaji wa Kenya kwa jinsi walivyocheza soka la hali ya juu.

Adebayor alisema kuwa Hassan ni ‘world class player’ anayeweza kutingisha dunia akipata fursa ya kuchezea timu kubwa zilizo maarufu na akaahidi kuendelea kuwasiliana naye mara kwa mara kwa ajili ya kumfanyia mipango ambayo hakutaka kuyataja wazi.

“Tungependelea Adebayor amtafutie kijana wetu Hassan timu kubwa huko barani Ulaya ili apate kutambulika na kuinua kipaji cha uchezaji wake. Tunaamini akipata timu maarufu, jina lake Hassan litapata kutambulika kote duniani kwa haraka,” amesema aliyekuwa mchezaji wa Burnley Amateur, Said Barex.

Barex amesema kuwa kijana huyo anaonekana kuwa mwiba kwa wapinzani na akamtaka kocha Jacob “Ghost” Mulee awe akimchagua kwenye kikosi cha timu ya taifa kwani ni mchezaji mwenye uwezo wa kupiga chenga na kufunga mabao.

“Tunaamini kama Hassan anaweza kuisaidia timu yetu ya Bandari kufanya vizuri kwenye mechi za Ligi Kuu ya FKF na kuinua jina la Harambee Stars katika mechi za kimataifa na hasa zijazo za kufuzu kwa dimba la Kombe la Dunia,” akasema Barex.

Naye aliyekuwa straika wa West Ham United FC, Ibrahim Khamis Zito anasema anavyocheza Hassan anamkumbusha wakati wake alipokuwa winga wa timu yake hiyo. “Ninaamini kwa soka la kisasa, Hassan anaweza kufika mbali kwani kuna maskauti wanamwangalia,” akasema Zito.

You can share this post!

‘Nimeandaa mapishi 25 kutoka nchi mbalimbali Afrika...

Nilikataa chanjo ya masonko nikachanjwa ile ya...