Michezo

Kiungo wa Everton kusalia mkekani kwa miezi 6

June 4th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO Jean-Philippe Gbamin wa Everton na timu ya taifa ya Ivory Coast sasa atasalia mkekani kwa kipindi cha miezi sita zaidi kuuguza jeraha baya la misuli ya mguu alilolipata akiwa mazoezini.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 alisajiliwa na Everton kutoka kambini mwa Mainz ya Ujerumani kwa kima cha Sh3.5 bilioni msimu wa 2018-19 ila akapata jeraha la kifundo cha mguu lililomweka nje kwa miezi tisa.

Hadi kufikia sasa msimu huu, amepangwa katika kikosi cha kwanza cha Everton kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mara moja tangu apate jeraha jingine la paja lililohitaji upasuaji.

Mapema wiki hii, Gbamin alisisitiza kwamba aliazimia kurudi katika hali yake ya zamani ya ubora wa fomu kabla ya kipute cha EPL kurejelewa msimu huu. Ndoto hiyo kwa sasa imezimika.

Hadi alipoumia, alikuwa akishiriki mazoezi katika kambi ya mazoezi ya Everton uwanjani Finch Farm chini ya kocha Carlo Ancelotti ambaye ameshikilia kwamba malengo yao ni kufuzu kwa kampeni za Europa League msimu ujao.

“Ni jeraha baya ambalo madaktari walikuwa awali wakikisia kwamba litaniweka nje ya kwa takrina miezi tisa. Ni matumaini yangu kwamba nitapona chini ya kipindi hicho na kurejea kwa kampeni za msimu ujao. Ilivyo dalili zote zinaashirikia kwamba nitakosa michuano yote iliyosalia msimu huu,” akasema Gbamin.