Kiungo Wyvonne Isuza astaafu soka

Kiungo Wyvonne Isuza astaafu soka

NA AREGE RUTH

KIUNGO mstaafu wa Harambee Stars Wyvonne Isuza anasema ataishi kukumbuka enzi zake akicheza soka.

Alisema hayo baada ya kutangaza kustaafu. Isuza, 28, alitangaza kustaafu mapema siku ya Jumamosi jioni chini ya mwezi mmoja tangu Shirika la Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (ADAK) kuweka hadharani kwamba lilimpiga marufuku ya miaka minne kujihusisha na soka tangu Septemba 2021 kwa kukiuka sheria za kupambana na pufya.

“Ulikuwa wakati mzuri wa kudumu,”  Isuza aliweka kwenye kurasa za akaunti zake katika mitandao ya kijamii siku ya Jumamosi na picha ya buti za kandanda zikiwa zimening’inia kwenye kamba.

ADAK ilikuwa imesema kuwa impiga marufuku baada ya Isuza kukataa, bila uhalali wa kulazimisha kuchukuliwa kwa sampuli yake kwa ajili ya majaribio, kama inavyotakiwa na Kanuni ya Dunia ya Kupambana na Matumizi ya Dawa za Pufya mwaka uliopita..

Katika ujumbe wake mfupi kwa Taifa Jumapili , kiungo huyo mshambuliaji alisema maisha yake ya soka ni “ya kukumbukwa” na kwamba sasa anachukua muda wake kukaa na familia yake nyumbani.

Alisema hayuko tayari kutoa maoni yake kuhusu marufuku yake ya ADAK.

“Nitazungumza kuhusu ADAK siku moja na sio leo,” alisema kiungo huyo ambaye alikuwa anaipigia klabu ya  Bandari baada ya kujiunga na klabu hiyo Oktoba 2021. Kila nilipoenda uwanjani kucheza ni mafasi  ambayo nilichukua na moyo wangu wote, ni mambo mazuri ya kukumbuka siku jizao.”

“Mnapaswa kujua kwamba kila kitu kinafika mwisho na mipango yangu sasa ni familia, familia na familia yangu pekee,” aliongezea Isuza.

Mnamo tarehe 14 Novemba, 2022, Bandari FC iliahidi kutoa taarifa kuhusu Isuza baada ya madai ya ADAK ya kutumia dawa za kusisimua misuli.

Isuza alichezea klabu zingine kadhaa humu nchini wakiwemo vigogo AFC Leopards, Wazito, Mathare United, Nairobi Stima na Thika United.

Alikuwa sehemu ya kikosi cha Harambee Stars kilichonyakua Kombe la Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) Senior Challenge makala ya mwaka 2017 yaliyofanyika nchini Kenya.

Alifunga bao la pekee lililoihakikishia Harambee Stars ushindi muhimu wa 1-0 dhidi ya Burundi kwenye nusu-fainali.

You can share this post!

Kocha Southgate aogopa kikosi cha Senegal

Raila ataka mradi wa Galana Kulalu usimamiwe na serikali za...

T L