Habari Mseto

Kiunjuri aashiria kuunga mkono mswada wa BBI

November 29th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri amebadilisha msimamo na kutangaza kuwa anaunga mkono marekebisho ya Katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI).

Akiongea Jumapili baada ya kuhudhuria ibada katika kanisa moja katika eneobunge la Laikipia Magharibi, Bw Kiunjuri ambaye ni mwandani wa Naibu Rais William Ruto ameunga mkono mabadiliko yaliyofanyiwa mswada wa BBI uliozinduliwa mnamo Jumatano katika jumba la KICC, Nairobi.

“Mswada wa BBI uliozinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga katika Bomas mnamo Oktoba 26 ulifanyiwa mabadiliko kwa kujumuishwa kwa masuala ambayo wananchi wengi walitaka. Hii ndiyo maana ninaunga mkono mswada wa sasa,” amesema.

Bw Kiunjuri ambaye ni kiongozi wa chama cha The Service Party (TSP) haswa ameunga mkono pendekezo la kubuniwa kwa maeneobunge 70, ambapo Kaunti ya Laikipia itapata eneobunge moja zaidi.

Hata hivyo, nwanasiasa huyo amesema chama cha TSP kinashauriana na viongozi na wanachama wake na kitatoa msimamo wake rasmi kuhusu suala zima la marekebisho ya Katiba.

“Tunausoma huu mswada. Tutauchambua kwa undani, tuongee na watu wetu kisha tutoe uamuzi. Ikiwa tutaridhika kuwa masuala yote tata yameshughulikiwa, tunavyoona, basi hatutakuwa na budi ila kuunga mkono,” akasema.

Akaongeza: “Tayari tumekubaliana kuwa maeneobunge mapya yanakuja na fedha. Wabunge hao hawatakuwa vikaragosi tu. Kwa mfano, hapa Laikipia tumepata eneo bunge moja zaidi ambayo itakuwa na fedha zaidi ya maendeleo.”

Mwanasiasa huyo alikuwa miongoni mwa wandani wa Dkt Ruto ambao walikuwa wameapa kuangusha mswada wa BBI ikiwa hautajumuisha masuala ambayo Wakenya wanataka.

Kauli ya Bw Kiunjuri imejiri baada ya Dkt Ruto mnamo Ijumaa kusema kuwa mswada huo umejumuisha masuala yaliyoibuliwa na Wakenya, hali iliyoashiria kuwa huenda akaunga mkono mswada huo katika kura ya maamuzi.

“Kipengele kipya cha 11A katika mswada wa marekebisho ya katiba kupitia BBI kitaendeleza masuala ya kiuchumi ya Wakenya wa kawaida. Kinatetea kitega uchumi cha walalahoi kama wenye kutumia wilbaro, bodaboda, mama-mboga, na wafugaji na kuhakikisha mapato kwa wakulima wa majanichai, kahawa, miwa, korosho, mahindi, miongoni mwa mazao mengine. Kipengele hicho kinainua uchumi wa ngazi ya mashinani,” Dkt Ruto akasema kupitia Twitter.

Hata hivyo, mnamo Jumamosi akijibu madai kuwa amebadili msimamo wake na kuamua kuunga mkono BBI, Dkt Ruto aliamua kusalia katika hali ya uvuguvugu, kwa kuchelea kufafanua waziwazi ikiwa anaunga mkono BBI au atapinga.

Akasema: “Ni wajibu wangu wa kikatiba kumsaidia bosi wangu, Rais. Tumeboresha BBI baada ya uzinduzi wa Bomas. Sasa tunajizatiti kusaka muafaka kwa manufaa ya Wakenya ili wapige kura isiyoleta migawanyiko. Tunataka kuepuka hali ambapo kuna waliopoteza na kuna wale walioshinda,” akasema kupitia Twitter.