Habari

Kiunjuri abanwa kwa kona

November 2nd, 2018 3 min read

BENSON MATHEKA Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri anakabiliwa na masaibu tele tangu alipoteuliwa kusimamia wizara hiyo katika kile kinachoonekana kuwa hujuma kutoka kwa maafisa wa idara zilizo chini yake, ili aonekane ameshindwa na kazi.

Matukio ya hivi majuzi yamemfanya waziri huyo kuonekana mtu asiye na uwezo wa kutekeleza majukumu yake licha ya kuwa ana mamlaka makubwa kama waziri.

Moja ya matukio hayo ni aibu ambayo imempata baada ya Bodi ya Nafaka (NCPB) kupuuza agizo lake la kuwauzia wasagaji mahindi gunia la kilo 90 kwa Sh1,600, ili kuwawezesha nao kuuza unga kwa Sh75 kwa pakiti ya kilo mbili.

Hali hii imefanya wasagaji kulalamika kuwa NCPB imemakataa kuwauzia mahindi kama walivyokubaliana na Bw Kiunjuri mnamo Septemba, na hivyo itawabidi kuuza pakiti ya kilo mbili ya unga wa mahindi kwa Sh100 ama zaidi.

Tukio hili limeaibisha sio tu Bw Kiunjuri, mbali hata Serikali yote kwa jumla kwa kutoa ahadi hewa.

Suala lingine ambalo limejitokeza kuwa hujuma dhidi ya Bw Kiunjuri ni hatua ya maafisa wa wizara yake kukosa kumfahamisha kuhusu ripoti ya Mamlaka ya Ubora wa Bidhaa (KEBS), ambayo inaeleza kuwa asilimia 60 ya mahindi katika maghala ya NCPB yameharibika na hayafai kuliwa na binadamu.

Kwenye kikao na kamati ya Seneti kuhusu Kilimo mnamo Jumatano, Waziri Kiunjuri alisema hakuwa na habari zozote kuhusu ripoti hiyo, licha ya maafisa wa KEBS, ambao pia walikuwa mbele ya kamati hiyo, kusema waliiwasilisha kwa maafisa wa wizara yake mnamo Oktoba 5.

Kulingana na ripoti ya KEBS, kuharibika kwa mahindi hayo kutasababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh7.6 bilioni.

Bw Kiunjuri alisema alisikia kuhusu ripoti hiyo kwa mara ya kwanza ilipotajiwa kwenye kikao hicho cha Jumatano. Hii inaibua maswali kuhusu ikiwa alikosa kufahamishwa ripoti hiyo kimakusudi, ilhali inahusu shirika lililo chini ya wizara yake. Pia ilimwonyesha kama mtu asiye na ufahamu kuhusu yanayoendelea katika wizara yake, ambayo ni ishara ya udhaifu.

Jana, mbunge Nandi Hills, Afred Keter alimtaka Bw Kiunjuri kujiuzulu kuhusiana na ripoti hiyo ya mahindi mabovu. Alimpa makataa ya siku saba kung’atuka la sivyo atawasilisha hoja ya kumwondoa afisini bunge litakaporejelea vikao vyake Jumanne wiki ijayo.

Duru zimedokeza kuwa Bw Kiunjuri, ambaye alichukua usukani katika wizara hiyo Februari mwaka huu, anahujumiwa na maafisa wanaohisi kwamba anatoka eneo lisilo muhimu hasa kwa kilimo cha mahindi.

Wadadisi wanasema pia kuna magenge yenye nguvu ambayo yana mizizi katika Wizara ya Kilimo, na ndiyo yanayochochea misukosuko katika wizara hiyo ili kuhakikisha Bw Kiunjuri ametimuliwa.

Magenge haya yamehusishwa na uagizaji wa sukari na mchele wenye sumu, mbolea feki na uuzaji wa mbolea ya bei nafuu kwwa wafanyibiashara kabla ya kumfikia mkulima na yamehusishwa na watu wenye nguvu serikalini.

Huku akigongwa na mawimbi makali hasa kuhusiana na mahindi, waziri anakabiliwa na shinikizo kutoka kwa bosi na rafiki yake, Rais Uhuru Kenyatta, ambaye amemuonya hadharani mara mbili kuhusu utepetevu katika wizara yake.

Pia katika ngome yake ya Mlima Kenya, wakulima wa kahawa nao wanataka majibu kuhusu iliko mbolea ya bei nafuu iliyonunuliwa na serikali kwa Sh1.9 bilioni. Wakulima hao wanasema licha ya kuahidiwa mbolea hiyo ili kuboresha kilimo cha kahawa, haijawafikia.

“Licha ya kupewa mamlaka na rasimali zote zinazotajika, ameshindwa kukabiliana na magenge ambayo yanavuruga sekta ya mahindi kwa hivyo anafaa kujiuzulu mara moja ili kutoa nafasi kwa watu wengine kusimamia wizara hiyo,” Bw Keter alisema alipohutubia kikao cha wanahabari katika majengo ya bunge.

“Changamoto kubwa katika wizara sio walaghai na wahusika wengine wa ufisadi bali ni utepetevu wa Waziri Kiunjuri. Iweje magunia milioni nne ya mahindi yanayohifadhiwa na NCPB yana sumu ya aflatoxin ilhali watu waliowasilisha mahindi hayo hawajachukuliwa hatua za kisheria?” akauliza.

Bw Keter alimtaka Bw Kiunjuri kuhakikisha kuwa mahindi hayo mabovu yanaondolewa katika maghala ya serikali haraka iwezekanavyo ili kuhakikisha kuwa hayauziwi Wakenya wasio na ufahamu.

“Hatua za haraka zinapasa kuchukuliwa ili kuzuia madhara ambayo yanaweza kutokana na hatua ya watu fulani kuanza kusambaza mahindi hayo kwa wasagaji wadogo wasio waangalifu hali ambayo itapelekea Wakenya kuathirika kiafya. Mahindi hayo pia hayafai kuuziwa watengenezaji lishe ya ng’ombe kwa sababu kiwango chake cha sumu haijulikani,” akasema.

Mbunge huyo alisema habari ya kuwepo kwa mahindi mabovu na malalamishi kutoka baadhi ya wasagaji kwamba bei ya mahindi imeanza kupanda ni njama ya watu kutoa sababu ya kuagizwa kwa mahindi kutoka ng’ambo kwa mara nyingine.

“Wakati huu hatutaruhusu hata punji moja ya mahindi kuingizwa nchini kutoka nje. Serikali inunue mahindi kutoka kwa wakulima wetu ambao wamepata mavuno mazuri mzimu huu,” akasema.