Habari Mseto

Kivuko cha Likoni sasa kuwekwa CCTV

August 16th, 2018 1 min read

Na KAZUNGU SAMUEL

UJENZI wa kituo cha kudhibiti kamera za usalama (CCTV) katika Kivukio cha Likoni utachukua miezi minne kukamilika, limesema Shirika la Huduma za Feri Kenya (KFS).

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Bw Bakari Gowa alisema kwa jumla, mradi huo utagharimu Sh95 milioni.

Kwenye mahojiano, Bw Gowa alisema kuwa uwekaji wa kamera hizo utakamilika katikati ya mwezi ujao, huku kituo cha kuzidhibiti kikitarajiwa kukamilika mwezi Desemba.

“Mradi wote utagharimu Sh95 milioni, zitakazojumuisha uwekaji wa kamera hizo katika feri zetu na afisi zote,” akasema.

Akaongeza: Ijapokuwa uwekaji wa kamera hizo hautachukua muda mrefu, ujenzi wa kituo cha kuzidhibiti utachukua kati ya miezi mitatu na minne kutoka sasa.”

Mwezi uliopita, kundi kutoka halmashauri hiyo lilizuru China kukagua utengenezaji wa kamera zitakazowekwa katika feri ambazo zitakuwa zikihudumu katika vivukio vya Likoni na Mtongwe.

Mkurugenzi huyo alisema kamera hizo zitaimarisha usalama katika feri hizo.

“Kamera zitawawezesha maafisa wa usalama kufuatilia kwa kina mienendo ya feri kwa urahisi,” akasema.

Bw Gowa alisema msongamano wa magari katika kivukio hicho chenye shughuli nyingi ulipungua kutoka magari 5,800 hadi 5,400 kwa siku mnamo Julai, lakini idadi hiyo imeanza kuongezeka.

“Mwanzoni mwa mwezi Julai, idadi ya magari ilipingua, ila yameanza kuongezeka tena. Kwa wastani, watu 340,000 hutumia kivuko hicho kila siku,” akaongeza.

Bw Gowa aisema kuwa halmashauri hiyo ilikua ikingoja baraza la mawaziri kupitisha pendekezo la kuwekwa kwa magari maalum ya kuvuta mizigo. Mradi huo ulipitishwa mnamo Jumanne, na utagharimu Sh4.1 bilioni.

Mradi wa magari hayo umepangiwa kuchukua miaka miwili.