KIVULI CHA BABA YAKE

KIVULI CHA BABA YAKE

Na WANDERI KAMAU

RAIS Uhuru Kenyatta anaonekana kumwiga baba yake, Mzee Jomo Kenyatta, na mwalimu wake wa kisiasa marehemu Daniel arap Moi, katika kila hatua ya maandalizi ya mchakato wa urithi wake mwaka 2022.

Wadadisi wanasema Rais anatumia mbinu sawa na alizotumia Mzee Kenyatta kulainisha taratibu za kumkabidhi mamlaka rais wa pili, Daniel Moi.

Rais Kenyatta anatarajiwa kung’atuka uongozini mwaka ujao baada ya kuhudumu kwa mihula miwili tangu 2013.

Baadhi ya mbinu alizotumia Mzee Kenyatta ni kumkabili yeyote aliyemwona kama mpinzani wake katika chama cha Kanu, kuingilia Bunge la Kitaifa na Seneti katika kushinikiza mageuzi ya kikatiba, kuzima uasi ulioibuka katika ngome yake ya Mlima Kenya na kuendesha mipango yake yote ya urithi katika ikulu.

Mzee Kenyatta vilevile alikuwa na kundi la wanasiasa waliokuwa karibu naye, waliodaiwa kumpa ushauri muhimu wa kisiasa.

Wanadaiwa kuhusika pakubwa kwenye mchakato huo. Tangu handisheki kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga mnamo 2018, miongoni mwa waathiriwa wakuu ni wanasiasa walioonekana kumwasi Rais na kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto.

Kama njia iliyofasiriwa kama mbinu ya “kuwapiga mjeledi”, wanasiasa hao waliondolewa kwenye kamati muhimu katika Seneti na Bunge la Kitaifa.

Baadhi yao ni maseneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Susan Kihika (Nakuru), Irungu Kang’ata (Murang’a) kati ya wengine.

Bw Murkomen na Bi Kihika walipoteza nafasi za Kiongozi wa Wengi katika Seneti na Kiranja wa Wengi kwenye Seneti mtawalia.

Vivyo hivyo, Mzee Kenyatta hakuwavumilia viongozi walioonekana kumkabili ama kumkosoa kwa namna yoyote ile.

Kwa mfano, Mzee Kenyatta alimfurusha mwanasiasa Bildad Kaggia kutoka Kanu baada yao kutofautiana kuhusu utaratibu wa ugavi wa mashamba nchini.

Mzee Kenyatta pia anadaiwa kuwa na usemi mkubwa kwenye harakati za kumwondoa Jaramogi Oginga Odinga kutoka Kanu.

Baadaye, Kaggia alijiunga na chama cha Kenya People’s Union (KPU) alichobuni Jaramogi baada ya kufurushwa kutoka Kanu.

“Lengo la (Mzee) lilikuwa kubuni mazingira ambapo mikakati yake ya kisiasa ilifaulu bila pingamizi yoyote.

Hangemvumilia mtu yeyote aliyeonekana kuwa kikwazo kwa mikakati hiyo hata kidogo,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni mwanahistoria na mdadisi wa siasa.

Mara tu baada ya kuchukua uongozi, Mzee Kenyatta aliendesha mageuzi makubwa ya kikatiba kwa kutoa maagizo kwa Bunge kuyatekeleza.

Baadhi ya mageuzi hayo yalilenga kuimarisha udhibiti wake katika Kanu au kuwaadhibu wapinzani wake kisiasa.

Mnamo Mei 1966, Bunge lilifanya mageuzi ya kikatiba kumpa Rais mamlaka kuagiza mtu yeyote aliyeonekana kama tishio la usalama kuwekwa kizuizini bila kufanyiwa kesi.

Ili kupanua uungwaji mkono wa kisiasa, alimteua Jaramogi kama makamu wa rais.

Mwaka uo huo, Bunge lilipitisha mageuzi ya kikatiba kumpa Rais usemi na mamlaka kuwateua maafisa wote muhimu katika Idara ya Utumishi wa Umma (PSC). Mnamo 1969, Bunge lilipitisha mageuzi ya kikatiba kumpa Rais mamlaka kuwateua makamishna wote wa Tume ya Uchaguzi Kenya (ECK).

Wadadisi wanasema mtindo uo huo ndio anaoiga Rais Kenyatta katika kushinikiza kupitishwa kwa mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI), kukiuka maagizo ya mahakama na kuingilia utendakazi wa Idara ya Mahakama.

“Mzee Kenyatta hangekabiliwa na yeyote kisheria. Alikuwa sahihi kwa lolote alilotenda.

Hakuna jaji ama hakimu angekosoa kitendo chake,” asema Bw Wamitu Ndegwa, ambaye ni msomi wa masuala ya sheria.

Kutokana na suitafahamu iliyokuwepo katika ukanda wa Mlima Kenya kuhusu urithi wake, Mzee Kenyatta alimtumia Mwanasheria Mkuu Charles Njonjo kuwakabili vikali wanasiasa waliojitokeza kupinga Daniel Moi kama mrithi wake.

Wanasiasa waliojitokeza katika ukanda huo kumpinga Mzee Moi walibuni vuguvugu la Change the Constitution Movement kuhakikisha “uongozi wa nchi haukuiponyoka Mlima Kenya.

” Wanasiasa waliojipata pabaya ni Kihika Kimani, Njenga Karume na wengineo.

Bw Njonjo alitoa onyo kali kwa yeyote “aliyempinga Mzee Moi, kwani alikuwa chaguo la Mzee Kenyatta.

” Sawa na babake, Rais Kenyatta amekuwa akiwakabili vikali wanasiasa kutoka Mlima Kenya wanaoonekana kupinga karata za urithi wake.

Wanasiasa ambao wamejipata pabaya ni wale wa mrengo wa ‘Tangatanga’ na chama cha UDA, kinachohusishwa na Dkt Ruto.

Polisi wamekuwa wakivuruga mikutano ya wanasiasa hao kwa kisingizio cha kutozingatia kanuni za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Mrengo huo umekuwa ukidai “kuonewa” na serikali. Sawa na babake, Rais Kenyatta amekuwa akiendesha masuala muhimu yanayohusu urithi wake kwenye Ikulu ya Nairobi ama Ikulu ndogo zilizo katika sehemu tofauti nchini.

Mnamo Februari, alifanya kikao na ya wajumbe 5,000 kutoka Mlima Kenya katika Ikulu Ndogo ya Sagana kuweka taratibu za kuipigia debe BBI.

Huo ndio umekuwa mtindo wake anapokutana na jumbe mbalimbali ama anapofanya ziara katika sehemu tofauti nchini kama Pwani, Magharibi, Nyanza na Bonde la Ufa.

Mchanganuzi wa siasa Godfrey Sang anataja mtindo huo kama mbinu ya Rais Uhuru kuzua taswira kwamba bado anadhibiti taratibu za urithi wake.

“Inaonekana Rais analenga kufanya kila awezalo kuhakikisha ana usemi kwenye mchakato mzima wa urithi wake licha ya kuonekana kupoteza ushawishi katika ngome yake,” asema Bw Sang.

You can share this post!

Kufa ghafla kwa TB Joshua kwawashtua wafuasi wake

Mbunge ashinikiza uchunguzi kuhusu dhuluma kwa wazee