Michezo

Kivumbi Butterfly ikitanua mabawa wikendi

May 23rd, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

KIVUMBI Kikali kinatazamiwa kushuhudiwa wikendi hii kwenye mfululizo wa mechi za Kundi C Ligi ya Taifa Daraja ya Pili huku Butterfly FC ikisaka alama tatu muhimu.

Butterfly FC ya kocha, Bernard Shikuri Jumapili itakuwa ugenini kucheza na Gogo Boys kwenye patashika itakayochezewa uwanjani Woodley Kibera, Nairobi.

Butterfly FC inalenga kushinda wenyeji wao kama ilivyotenda kwenye mechi za mkumbo wa kwanza. Kwenye mechi za mkondo wa kwanza Butterfly ilizoa mabao 2-1 dhidi ya Gogo Boys.

”Hata hivyo hatuwezi kubashiri mchezo huo maana wapinzani wetu watakuwa katika ardhi ya nyumbani,” meneja wa Butterfly, Fredrick Ndinya alisema na kuongeza kuwa hawana lingine ila wamepania kuvuna alama zote muhimu ugenini.

Nao vinara wa kipute Gor Mahia Youth itakuwa katika Uwanja wa Camp Toyoyo Jericho, Nairobi kukaribisha Kibera United. Gor Mahia Youth itakuwa mbioni kuwinda alama zote ili kuendelea kujiongezea matumaini ya kuibuka mabingwa wa kundi hilo na kufuzu kupandishwa ngazi msimu ujao.

Kwenye ratiba hiyo, MKU Thika iliyo katika mduara wa kushushwa ngazi itakuwa nyumbani kuialika CMS Allstars huku ikilenga kuvuna alama tatu muhimu kwenye juhudi za kujiondoa katika hali hiyo.

MKU Thika itapanda hatua moja na kujiondoa katika mduara wa kuteremhswa ngazi endapo itashinda mchezo huo nayo Kibra United ishindwe na Gor Mahia Youth.

Katika jedwali la mechi hizo, Gor Mahia Youth inayosongolea kunasa tiketi ya kusonga mbele inaongoza kwa kufikisha alama 45.

Nayo Butterfly FC imekamata nafasi ya pili kwa kuvuna alama 38, moja mbele ya Tandaza baada ya kucheza mechi 18 na 19 mtawalia.