Siasa

Kivumbi chaanza Joho akitua Msambweni

October 17th, 2020 2 min read

Na MOHAMED AHMED

KIVUMBI kinatarajiwa katika uchaguzi mdogo wa Msambweni baada ya Gavana wa Mombasa, Hassan Joho na mwenzake wa Kwale, Salim Mvurya kuunga wagombeaji wawili wapinzani.

Huku Bw Joho akimuunga mkono mgombeaji wa chama cha ODM, Omar Boga, Bw Mvurya ametangaza yuko nyuma ya mgombeaji huru Feisal Bader ambaye pia anapigiwa debe na Naibu Rais William Ruto.

Viongozi wengine wa Kaunti ya Kwale ambao wako upande wa Bw Bader ni wabunge wa Khatib Mwashetani (Lunga Lunga), Benjamin Tayari (Kinango) na naibu wa Bw Mvurya, Bi Fatuma Achani.

Viongozi wengine ni pamoja na mbunge wa Malindi Aisha Jumwa, Owen Baya (Kilifi Kaskazini) Didmus Barasa (Kimilili) na waliokuwa maseneta Hassan Omar (Mombasa), Johnson Muthama (Machakos), Boni Khalwale (Kakamega) miongoni mwa wengine.

Baada ya Bw Bader kuwasilisha stakabadhi zake mnamo Alhamisi viongozi hao walifululiza pamoja na mgombea huyo katika uwanja wa Sawa Sawa eneo la Ramisi ambapo waliuza sera zake.

Viongozi hao walitaka wakazi kumpigia kura Bw Bader kama hisani kwa mjombake Bw Suleiman Dori ambaye alifariki na kuacha wazi kiti hicho ambacho kinapiganiwa saa hii.

“Sisi tulifanya kazi na Bw Dori na tumeona kuwa katika chaguzi ndogo za hapo nyuma ndugu za marehemu wanapewa kiti lakini hapa tunaona upande ule mwengine umedinda kufanya hilo, hivyo basi nawaomba mrejeshe hisani kwa familia hii,” akasema Bw Mwashetani aliyekuwa anaongoza mkutano huo.

Bw Tayari pia alisisitiza hilo na kusema kuwa licha ya yeye kuwa mwanachama wa ODM ameamua kumpigia debe Bw Bader kwa sababu ya hisani yake kwa Bw Dori.

Viongozi hao wengine pia walimpigia debe Bw Bader na kusema kuwa watakita kambi eneo hilo la Msambweni kuhakikisha kuwa wanaibuka washindi.

Kwa upande wao, viongozi wa ODM wakiongozwa na Gavana wa Mombasa Hassan Joho jana alisema kuwa watakita kambi eneo hilo kuhakikisha kuwa Bw Boga anashinda kiti hicho.“Sisi kama chama tupo tayari kwa ushindani huu.

Na ninaamini tutashinda kwa sababu tupo na ajenda kwa watu wa Msambweni. Bw Boga ndiye kiongozi anayestahili nafasi hiyo. Sisi hatushindani na watu ambao wanafanya siasa zao Nairobi,” akasema Bw Joho.

Bw Joho alimshambulia Dkt Ruto akisema kuwa kama yeye ni mkali kweli na anajiamini basi aende eneo la Pwani wapimane nguvu. Alisema kuwa yeye hatashindana na wale wanaotumwa na Dkt Ruto kwani hao ni watu ambao hawapo ngazi yake ya kisiasa.

Seneta James Orengo naye alisema kuwa Bw Boga atashinda kiti hicho kwa sababu eneo la Msambweni ni ngome ya ODM.“Tukiwa na Joho ndiye anaongoza kampeni na Boga kama mgombea wa ODM na handisheki basi tutashinda kiti hicho. Nawaomba tufanye kampeni za amani sisi sote,” akasema.

Bw Mvuvra ambaye ni gavana wa Jubilee alisema kwamba Bw Bader ndiye anayeweza kuwafaa wakazi wa Msambweni kwa sababu alifanya kazi kwa karibu na marehemu Dori.