Kivumbi chanukia ‘Tangatanga’ wakishiriki jukwaa moja na Raila

Kivumbi chanukia ‘Tangatanga’ wakishiriki jukwaa moja na Raila

ANTHONY KITIMO na CHARLES WASONGA

KIVUMBI chanukia Mombasa leo Jumamosi viongozi wa mrengo wa ‘Tangatanga’ watakapojibwaga kwenye jukwaa moja na kiongozi wa ODM, Raila Odinga katika mkutano wa hamasisho kuhusu mapendekezo ya ripoti ya mchakato wa maridhiano (BBI).

Licha ya waandalizi wa mkutano huo, wakiongozwa na Gavana Ali Hassan Joho, kutangaza kuwa wamekaribishwa mkutanoni lakini hawataruhusiwa kuhutubu, wafuasi hao wa Naibu Rais William Ruto wameapa kuhudhuria mkutano huo, liwe liwalo.

Ijumaa, kundi la vijana liliwashambulia wabunge wanne kutoka Pwani wanachama wa ‘Tangatanga’ walipokuwa wakiwahutubia wanahabari wakilalamikia kutelekezwa katika mipango ya mkutano huo.

Wabunge hao; Aisha Jumwa (Malindi), Mohamed Ali (Nyali), Athman Sheriff (Lamu Mashariki) na Getrude Mbeyu (Mbunge Mwakilishi, Kilifi) walisisitiza watafika katika mkutano katika bustani ya Mama Ngina Waterfront.

“Sisi tuko hapa ili kuhakikisha mkutano huo unafanyika kwa amani lakini kama hivi ndivyo BBI italeta utangamano, basi ni kinaya kwa zoezi hilo lote,” alisema Bi Jumwa nje ya mkahawa wa Lotus mjini Mombasa.

“Tumechaguliwa na wapwani na ni makosa makubwa kama tutanyimwa ruhusa kuongea wakati mkutano unafanyika kwetu,” akaongeza huku akikashifu vijana hao.

Naye Bw Mohammed alielekeza kidole cha lawama kwa Bw Joho akidai yeye ndiye aliwakodi vijana hao “kutushambulia kwa mawe.”

“Gavana Joho ambaye amewalipa vijana hawa afahamu kuwa kama Mkenya yeyote yule, Bi Jumwa pamoja nasi hapa tuna uhuru wa kusema yaliyo moyoni mwetu. Hamwezi kumshambulia kiongozi mwanamke kwa sababu ana msimamo tofauti,” akasema Bw Ali.

Naye Seneta wa Elgeyo Marakwet, Kichumba Murkomen alidai ametishiwa maisha kufuatia tangazo lake la kuhudhuria mkutano huo.

Murkomen ambaye ni kiongozi wa wengi katika Seneti alifichua kuwa amearifiwa kwamba kando na kunyimwa kiti mkutanoni, atanyimwa pia nafasi ya kuhutubia umati.

Katika ujumbe kupitia akaunti yake ya Twitter, Seneta huyo alisema kwa kejeli kwamba, yuko tayari kukabiliana na mawimbi hayo iwapo hiyo ndio njia pekee ya kuwaunganisha Wakenya.

“Nimearifiwa kuwa iwapo nitahudhuria mkutano wa BBI, nitadhulumiwa kwa kunyimwa kiti na nafasi ya kuzungumza. Iwapo hilo litaleta umoja basi ni sawa. Tukutane Mombasa,” Bw Murkomen akasema.

You can share this post!

MWANAMKE MWELEDI: Aweka kumbukumbu kuchaguliwa mbunge

TAHARIRI: Harambee wapeni Wakenya furaha

adminleo