Michezo

Kivumbi chatarajiwa EPL ikikamilika

July 25th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

LIGI Kuu ya Uingereza (EPL) ilirejelewa mnamo Juni 17, 2020 baada ya kusitishwa kwa zaidi ya miezi mitatu kutokana na janga la corona. Wakati huo, kila kikosi kilikuwa kimesalia na kati ya mechi tisa na 10 kukamilisha rasmi kampeni za msimu huu wa 2019-20.

Ililazimu wasimamizi kuratibu mingi ya michuano kusakatwa katikati ya wiki za Juni na Julai ili kufanikisha mpango wa kutamatisha msimu kufikia mwisho wa Julai na kupisha mapambano ya soka ya bara Ulaya.

Baada ya wiki moja pekee ya kurejelewa kwa EPL, Liverpool walijitwalia ubingwa wa muhula huu. Ushindi wa 2-1 uliosajiliwa na Chelsea dhidi ya Manchester City uwanjani Stamford Bridge mnamo Juni 25 uliwapa Liverpool taji lao la 19 walilolisubiri kwa miaka 30.

Masogora hao wa kocha Jurgen Klopp walilinyanyua kombe usiku wa Julai 22 baada ya kuwatandika Chelsea 5-3 uwanjani Anfield.

Msimu wa 2019-20 wa EPL unatamatika rasmi mnamo Julai 26, 2020 kwa mechi 10 zitakazotandazwa na klabu zote 20 kwa wakati mmoja (6:00pm).

Macho ya mashabiki yataelekezwa zaidi kwa Manchester United, Chelsea na Leicester City wanaopigania nafasi mbili za zilizoachwa na Liverpool na Manchester City ili kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao. Jicho jingine litakuwa likiwamulika Bournemouth, Watford na Aston Villa ambao watakuwa katika vita vya kuepuka shoka la kuwateremsha daraja. Norwich City ambao watakuwa wageni wa Man-City ugani Etihad, tayari wameshushwa ngazi ligini baada ya kupoteza mechi 26 kati ya 37 zilizopita.

Bournemouth watawaendea Everton uwanjani Goodison Park, Watford wavaane na Arsenal uwanjani Emirates nao Villa wapimane ubabe na West Ham United uwanjani London.

Man-United wanahitaji alama moja pekee katika mechi itakayowakutanisha na Leicester City uwanjani King Power ili kufunga msimu ndani ya mduara wa nne-bora na hivyo kufuzu kwa UEFA msimu ujao.

Sare ya 1-1 iliyosajiliwa na masogora hao wa kocha Ole Gunnar Solskjaer dhidi ya West Ham mnamo Julai 22 ugani Old Trafford iliwapaisha hadi nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 63 sawa na Chelsea watakaolazimika kuweka kando maruerue ya kupondwa na Liverpool watakaposhuka dimbani kukabiliana leo na Wolves ugani Stamford Bridge.

Ushindi kwa Leicester wanaonolewa na kocha Brendan Rodgers utawanyima Man-United nafasi ya kunogesha kivumbi cha UEFA iwapo Chelsea nao watawanyuka Wolves ambao kwa pamoja na Tottenham, wamejikatia tiketi za kushiriki Europa League msimu ujao.

Hata wakiwachabanga Watford, Arsenal watakamilisha kampeni za EPL msimu huu katika nafasi mbovu zaidi tangu 1995. Chini ya kocha Mikel Arteta, miamba hao wa zamani wa soka ya Uingereza hawawezi kukamilisha kampeni za muhula huu ndani ya mduara wa saba-bora, kumaanisha kwamba hawatakuwa sehemu ya vikosi vitakavyoshiriki kipute kijacho cha Europa League iwapo watashindwa kuwaangusha Chelsea kwenye fainali ya Kombe la FA mnamo Agosti 1 uwanjani Wembley, Uingereza.

RATIBA YA EPL (Julai 26, 2020 6:00pm):

Chelsea na Wolves

Leicester City na Man-United

Southampton na Sheffield United

Newcastle United na Liverpool

West Ham United na Aston Villa

Burnley na Brighton

Arsenal na Watford

Man-City na Norwich City

Crystal Palace na Tottenham

Everton na Bournemouth