Michezo

Kivumbi Kenya na Uganda zikifufua uhasama voliboli ya wanawake kuingia All-African Games 2019

May 21st, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE
Kenya na Uganda zitamenyana Jumanne (8.00pm) katika fainali ya mchujo wa voliboli ya wanawake ya Ukanda wa Tano wa kufuzu kushiriki mashindano ya Bara Afrika (All-African Games) katika ukumbi wa Lugogo jijini Kampala.
Malkia Strikers ilishinda Rwanda na Ethiopia kwa seti 3-0 kila mmoja nayo Uganda ililaza Ethiopia 3-0 na Rwanda 3-1 katika mchujo huu uliovutia mataifa manne baada ya tishio kubwa kwa Kenya, Misri, kujiondoa dakika ya mwisho.
Baada ya Kenya kuandikisha ushindi wa pili mfululizo bila kupoteza seti, kocha mkuu wa mabingwa wa Kenya, Prisons, Josp Barasa alisema Jumatatu, “Ni mechi iliyoegemea upande mmoja kwa sababu tulidhibiti kila idara. (Triza) Atuka alifanya kazi nzuri ya kuzuia makombora yao. Lorine (Chebet) alitatiza sana Ethiopia kupitia “service” zake nao (Mercy) Moim na (Janet) Wanja walipeana pasi murwa.”
Kuhusu mechi kati ya Kenya na Uganda, Barasa alikuwa amesema katika mahojiano ya awali kwamba itakuwa ngumu. Alikiri kwamba timu ya Uganda ya wakati huu ni tofauti sana na ile iliyokuwepo miaka miwili iliyopita. “Waganda wameimarika sana na hatuwezi kuwachukulia kwa urahisi,” Barasa alieleza Taifa Leo.
Kenya haijawahi kupoteza dhidi ya Uganda na inatarajiwa kuendeleza rekodi hiyo yake nzuri Juamnne usiku na kufuzu kutetea taji la All-African Games ililoshinda baada ya kubwaga Cameroon 3-1 katika fainali ya mwaka 2015 jijini Brazzaville, Congo.
Mshindi kati ya Kenya na Uganda ataingia mashindano ya All-African Games yatakayofanyika mjini Rabat nchini Morocco mnamo Agosti 19-31, 2019. Mechi hii imetunguliwa na ile kati ya Rwanda na Ethiopia hapo saa kumi na mbili jioni.