Kiwanda cha mananasi kujengwa Gatundu Kaskazini

Kiwanda cha mananasi kujengwa Gatundu Kaskazini

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Gatundu Kaskazini wana sababu ya kutabasamu baada ya kuahidiwa na serikali ya Kaunti ya Kiambu kuwa watajengewa kiwanda cha mananasi.

Kwa muda mrefu wakazi hao wamekuwa wakizalisha matunda hayo lakini hawana mahali maalum pa kuyapeleka kwa manufaa ya kibiashara.

Ina maana kwamba wafanyabiashara wengi kutoka sehemu za mbali ndio hunufaika na mananasi hayo kwa kuyanunua kwa bei ya chini huku wakijinufaisha kwa kuyauza kwingineko.

Tayari serikali ya Kaunti ya Kiambu imetenga takribani Sh20 milioni kugharimia ujenzi wa kiwanda hicho.

Kulingana na mipango ya kaunti hiyo, wataalam wako mashinani ili kuhoji wakazi wa eneo hilo na kupanga mikakati kabambe ni lini mradi huo utang’oa nanga.

Mkazi wa eneo hilo Bw Francis Kamau alielezea furaha yake kuhusu mpango huo akisema ni afueni kwa wakulima wa mananasi Mang’u, Githobokoni, na Kamwangi.

Kwa wakati huu, Kaunti ya Kiambu ikishirikiana na wahandisi wakuu inaendelea kufanya mikakati ili kujua eneo halisi litakalofaa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho.

Mkazi mwingine wa huko, Bi Margret Wangari Kamau, amekiri ya kwamba matunda hayo yalikuwa yakiharibikia shambani kwa wingi kwa kukosa soko.

“Wakulima wengi walilazimika kuuza zao hilo kwa bei ya chini huku wakikosa kupata faida yoyote,” alifafanua Bi Kamau.

Kwa hivyo, wakazi hao wamekiri kuwa pendekezo la kupata kiwanda kipya eneo la Gatundu litabadilisha hali ya biashara kwa watu wengi.

Mkulima Bi Alice Muthoni amesema kiwanda kipya kikijengwa kitabadilisha kabisa maisha ya wakazi wa Gatundu Kaskazini na vitongoji vyake.

“Sisi kama wakazi wa Gatundu tutapata faida mkubwa kwa sababu tutauza zao letu kwa kiwanda hicho,” alifafanua Bi Muthoni.

Matunda hayo yametajwa kama ya gredi ya juu kutokana na hali ya tabianchi ya upande huo na jinsi yanavyokuzwa.

You can share this post!

EACC yagonga mwamba katika uchunguzi kuhusu vyeti feki vya...

FUNGUKA: ‘Najua mtasema ni wazimu…!’