Habari

Kiwanda cha maziwa cha Daima chafungwa kwa uchafuzi wa Mto Nairobi

August 27th, 2019 1 min read

Na SARAH NANJALA

MAMLAKA ya Kuhifadhi Mazingira Nchini (Nema) imefunga kiwanda cha maziwa cha Sameer Daima kwa muda usiojulikana kwa kuchafua Nairobi River.

Meneja wa operesheni katika kiwanda hicho cha eneo la Viwandani jijini Nairobi Bw Kenneth Kareithii naye pia amekamatwa Jumanne kwenye msako ulioendeshwa na maafisa wa polisi waliokuwa wameandamana na maafisa wa Nema.

Kaimu mkurugenzi mkuu wa Nema, Bw Mamo B. Mamo ameahidi kuendelea kukabili kampuni na viwanda ambavyo vinamwaga uchafu katika mto huo wa Nairobi ambao zamani ulikuwa safi na wenye sifa nzuri.

“Nema imepata sehemu 122 za uchafuzi wa Mto Nairobi. Kwenye uchunguzi uliofanywa, asilimia 50 ya kampuni zimetii masharti na sera. Msako wa sasa ni wa kuhakikisha asilimia iliyosalia inatii kanuni ya Kudhibiti Ubora wa Maji ya 2006 la sivyo hatua za kisheria zichukuliwe na maafisa wake kushtakiwa,” amesema Bw Mamo.

Maafisa wa Nema pia wamefanya msako katika kampuni ya kemikali ya Synresins inayotengeneza malighafi muhimu katika kutengeneza rangi, wino na vitambaa na kumkamata Afisa Mkuu Mtendaji Mira Shah, meneja wa uzalishaji bidhaa Michael Mungai na mkuu wa nguvukazi Yvonne Nyokabi. Kampuni hiyo imefungwa kwa kuachilia uchafu hatari katika laini ya majitaka na kuchafua mazingira.

Mnamo Jumatatu, Nema ilifunga Modern Lithographic (K) Ltd, na Apex Limited (zinazotengeneza rangi), Thorlite Kenya Ltd na Kamongo Paper Recycling Company, zote zikiwa Eneo la Viwandani.

Kufikia sasa jumla ya viwanda 53 vimefanyiwa msako.

Haya yanajiri majuma machache baada ya Taifa Leo na Daily Nation kuchapisha msururu wa makala kuangazia kadhia ya uchafuzi mazingira katika Mto Nairobi.