Habari Mseto

Kiwanda chatimua watu 280

March 5th, 2020 2 min read

 Na STEVE NJUGUNA

USIMAMIZI wa kiwanda cha maziwa cha Nyahururu, Alhamisi uliwafuta wafanyakazi 280.

Hatua hiyo kulingana na wasimamizi inatokana na mageuzi mapya ya kisasa yanayotarajiwa kukumbatiwa kwenye oparesheni za kiwanda hicho.

Mkurugenzi Msimamizi, Bw Simon Mwanjang’i, alitangaza kwamba walikatiza kandarasi ya wafanyakazi hao baada ya kiwanda hicho kusimamisha shughuli zake kwa muda ili kutoa nafasi kwa mabadiliko hayo ya kuboresha utendakazi wake.

“Hii ni kuwajuza kwamba oparesheni za kiwanda zimesimamishwa ili kupisha mageuzi mapya ya kisasa. Usimamizi umeafikia kutamatisha kandarasi zenu mara moja,” ikasema sehemu ya barua hiyo ya Februari 29, 2020.

Hata hivyo, wafanyakazi waliotimuliwa walisema kwamba kiwanda hicho bado kilikuwa kikiendelea na shughuli zake na kukosoa usimamizi kwa kupotosha umma.

Msemaji wao, Bw James Mwangi alisema usimamizi haukutoa ufafanuzi wa kuridhisha uliochangia kutimuliwa kwao na wanashuku kuna jambo fiche ambalo hawajaelezwa.

“Hakuna sababu inayoridhisha ambayo imesababisha tufutwe kazi ilhali kiwanda kinaendelea na shughuli zake kama kawaida. Tunashuku kwamba kuna jambo fiche lililosababisha usimamizi kuafikia kwamba huduma zetu hazihitajiki tena,” akasema Bw Mwangi.

Alishangaa kwa nini wakulima bado walikuwa wameruhusiwa kupeleka maziwa yao kiwandani ilhali usimamizi ulikuwa umewaeleza kwamba oparesheni zote zimesitishwa.

Bw Mwangi pia alifichua kuwa wengi waliopigwa kalamu walikuwa wamefanya kazi kiwandani humo kwa muda mrefu bila kupokezwa ajira ya kudumu.

“Baadhi yetu wamefanya kazi kwa zaidi ya miaka 10 ilhali usimamizi ulikuwa umekataa kutupa ajira ya kudumu jinsi inavyotakikana kisheria. Iwapo shughuli za kiwanda zimesitishwa, kwa nini wakulima wanaruhusiwa kupeleka maziwa yao kiwandani?” akauliza.

Wafanyakazi hao walidai wenzao ambao walijiunga na kiwanda hicho majuzi walipewa ajira za kudumu huku wao wakipuuzwa. Walisema huo ulikuwa ubaguzi mkubwa na wangepokezwa nafasi hizo kwanza kisha zilizosalia zipatiwe waajiriwa hao wapya.

Kutimuliwa kwa wafanyakazi hao kunajiri wakati ambapo Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuzuru kiwanda hicho wiki ijayo ili kutathmini hatua zilizopigwa kutekeleza mradi wa kukipanua.

Mnamo Januari, Rais Kenyatta aliagiza kiwanda hicho kipokezwe Sh575 millioni za kugharimia upanuzi wake na Sh500 millioni zaidi kukiwezesha kununua maziwa kutoka kwa wakulima.

Kiwanda hicho ndicho kikubwa zaidi na hupokea maziwa kutoka kwa wafugaji wa ng’ombe za maziwa kutoka Kaunti za Nyandarua, Laikipia na Baringo.