Kiwanda kipya cha macadamia kuleta mabadiliko

Kiwanda kipya cha macadamia kuleta mabadiliko

NA LAWRENCE ONGARO

KUNA matumaini mema kwa wakulima wa zao la macadamia ambao walipata changamoto ya kuuza kwa masoko ya ng’ambo.

Kwa miezi michache iliyopita uuzaji wa macadamia katika bara Ulaya na masoko ya Amerika na Canada umekuwa na changamoto kwa wakulima wa Kenya.

Wataalam wa kilimo wanasema kabla ya kusafirisha zao hilo nchi za ng’ambo, ni sharti macadamia kuwa na kiwango kidogo cha pathojeni ili ubora uwe ni wa hali ya juu.

Baada ya wakulima kupitia masaibu hayo kampuni ya Jungle Nuts Ltd mjini Thika imeamua kujenga kiwanda kitakachogharimu Sh500 milioni ili kutosheleza mahitaji yote ya wakulima kabla ya kusafirisha nje zao la macadamia.

“Wakulima wengi wamejitokeza kupanda macadamia na hata wataalam wengi wa kilimo wamezuru maeneo mengi nyanjani kuwarai wakazi wa Kiambu na Murang’a kupanda macadamia kwa wingi,” akasema mkurugenzi wa kiwanda hicho Bw Patrick ‘Wa Jungle’ Wainaina.

Alisema kwa miezi michache iliyopita wakulima wamepitia changamoto tele kwa sababu nchi za ng’ambo zimewawekea vikwazo chungu mzima kabla ya kununua zao hilo katika soko la dunia.

“Kwa muda huo wa miezi michache, nchiĀ  za Ulaya zinataka zao hilo lisafirishwe nje likiwa limepitia ukaguzi wote muhimu kabla ya kupakiwa katika makatoni na kusafirishwa,” alisema Bw Wa Jungle.

Hata hivyo, mkurugenzi huyo ametoa wito kwa wakulima wote popote walipo wawe watulivu kwa sababu hivi karibuni kiwanda cha macadamia kitakamilika na kuanza kazi mara moja.

“Nina imani kampuni hiyo italeta afueni kwa wakulima wote wa macadamia kwa sababu itafuata mikakati yote ya kutayarisha zao hilo hadi kufikia hatua ya kupakiwa vizuri kwenye makatoni na kusafirishwa hadi kwa masoko ya kimataifa,” alifafanua mkurugenzi huyo.

Alisema kutokana na vikwazo hivyo bei ya macadamia imeshuka kutoka Sh200 hadi Sh100 kwa kilo moja.

Hata hivyo, Bw Wainaina aliyekuwa mbunge wa Thika amewahakikishia wakulima wasiwe na wasiwasi kwa sababu hayo yote yatakwisha na mambo yawe mazuri kwao.

Kulingana na mkurugenzi huyo, zao hilo linapandwa kwa wingi katika kaunti za Kiambu na Murang’a na kwa uchache katika kaunti nyingine chache zilizo karibu.

  • Tags

You can share this post!

Kocha Oyoo anoa nyota wa kesho

Pacha waliong’aa KCSE Pwani wafichua siri

T L