Michezo

Kiyara aunda milioni kwa muda wa saa mbili Taiwan

March 18th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MKIMBIAJI Rael Kiyara amejizolea Sh1, 012,240 baada ya kushinda mbio za New Taipei City Wan Jin Shi Marathon nchini Taiwan, Jumapili.

Kiyara alikuwa bega kwa bega na Chemtai Rionotukei hadi mita za mwisho kabla ya kulemea Mkenya huyu mwenzake utepeni.

Alinyakua taji kwa saa 2:35:57, sekunde moja mbele ya Rionotukei (2:35:58) naye Ji Hyang Kim (Korea Kaskazini) akafunga tatu-bora kwa saa 2:38:10.

Wakenya Rebecca Jepchirchir (2:39:59) na Salome Jerono (2:40:07) waliridhika katika nafasi za nne na tano, mtawalia. Nambari mbili hadi tano walituzwa Sh607,344, Sh404, 896, Sh303,672 na Sh202,448, mtawalia.

Mjapani Yuki Kawauchi alinyakua taji la wanaume kwa saa 2:14:12 akifuatwa unyounyo na Mkenya Johnstone Maiyo (2:14:40), Muethiopia Aredom Degefa (2:14:54), Mkenya Stanley Koech (2:21:28) naye Muethiopia Tsegaye Debele (2:21:50) akafunga tano-bora.

Rekodi za mashindano haya ya kilomita 42 ya New Taipei City Wan Jin Shi zinashikiliwa na Mkenya William Chebon (2:13:05) na Mkorea Ji Hyang Kim (2:34:52). Chebon aliweka rekodi ya wanaume mwaka 2016 naye Kim ameshikilia rekodi ya wanawake tangu mwaka 2014.