Michezo

Kiyeng ambwaga Chepkoech kwa mara ya kwanza

September 14th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MSHINDI wa nishani ya fedha katika Olimpiki za Rio 2016, Hyvin Kiyeng, alimpiku bingwa wa dunia, Beatrice Chepkoech kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitatu.

Hii ni baada ya Kiyeng kuibuka malkia wa mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwenye kivumbi cha ISTAF Berlin, Ujerumani mnamo Jumapili.

Wakenya hao wawili walikuwa unyo kwa unyo hadi kiunzi cha mwisho. Hata hivyo, Kiyeng aliyeibuka bingwa wa dunia mnamo 2015, alimpigia hesabu Chepkoech katika hatua ya mwisho na kufika utepeni kwa muda bora wa dakika 9:06.04

Kiyeng alimbwaga Chepkoech kwa mara ya mwisho mnamo 2017 walipotifua kivumbi cha Doha Diamond League. Miaka mitatu baadaye, mtimkaji huyo aliridhika na medali ya fedha katika mbio za World Athletics Tour zilizoandaliwa jijini Berlin, Ujerumani.

Wakishindana jijini Doha, Kiyeng, 28, aliandikisha muda wa dakika 9:00.12 na kumzidi ujanja Chepkoech aliyeambulia nafasi ya tatu kwa dakika 9:01.57. Ingawa hivyo, Chepkoech alijinyanyua na kuibuka mshindi wa Michezo ya Afrika iliyoandaliwa mjini Asaba, Nigeria mnamo 2018 kisha akavunja rekodi ya dunia kwa kukamilisha duru ya Diamond League jijini Monaco, Ufaransa kwa muda wa dakika 8:44.32 mnamo Agosti mwaka huo.

Mwaka uo huo, Chepkoech aliibuka mshindi wa Continental Cup kwa kutawala mbio za Ostrava nchini Czech kwa muda bora wa dakika 9:07.92 kabla ya kutawala Riadha za Dunia za 2019 jijini Doha, Qatar kwa muda wa dakika 8:57.84.

Mbio za Berlin mnamo Jumapili zilikuwa za kwanza kwa Kiyeng kushiriki msimu huu. Chepkoech, 29, alitarajiwa kujinyanyua na kutamba baada ya kutupwa hadi nafasi ya sita kwenye mbio za mita 5,000 zilizotamalakiwa na bingwa wa dunia na malkia wa Jumuiya ya Madola, Hellen Obiri, kwenye duru ya kwanza ya Diamond League msimu huu jijini Monaco, Ufaransa mnamo Agosti 14.

Chepkoech alikuwa pia amejinoa vya kutosha baada ya kunogesha kivumbi cha mita 1,500 kwenye mbio za World Indoor Tour jijini Dusseldorf, Ujerumani mnamo Februari 5, 2020.

Chepkoech ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji, alisajili muda bora wa msimu huu wa dakika 9:10.07 nchini Ujerumani na kuwapiku Marusa Mismas wa Slovakia (9:20.68).

Mkenya Mercy Chepkirui alikamilisha mbio za ISTAF Berlin mnamo Jumapili katika nafasi ya tisa kwa muda wa dakika 9:45.70.

Laura Muir aliboresha muda wake katika mbio za mita 1,500 kwa kusajili muda wa dakika 3:57.40 na hivyo kumbwaga Mwingereza mwenzake Laura Weightman (4:00.09). Jessica Hull wa Australia aliambulia nafasi ya tatu kwa dakika 4:00.42 – muda ambao ulikuwa rekodi mpya ya kitaifa na bara Asia.