Kizaazaa EFL Cup leo soka ikisonga mbele

Kizaazaa EFL Cup leo soka ikisonga mbele

LONDON, Uingereza

ROBO-FAINALI ya kombe la England Football League (EFL Cup), almaarufu carabao Cup, itasaktwa leo usiku huku mechi tatu kubwa zikitarajiwa kutifua kivumbi.

Tottenham Hotspur wataalika West Ham katika “Debi ya London” uwanjani Tottenham Stadium.Liverpool itakuwa mwenyeji wa Leicester City ugani Anfield.Nao Chelsea watakuwa wageni wa Brentford katika uga wa Brentford Community Stadium.

Mechi hizo za katikati mwa wiki zinasakatwa baada ya klabu za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kukubali kucheza mechi zao msimu wote wa sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya, licha ya wimbi jipya la corona kuteka taifa hilo.Uamuzi wa klabu hizo uliafikiwa Jumatatu jioni, siku chache tu baada ya wachezaji kadhaa na maafisa wa klabu kupatikana na virusi hivyo, vinavyosababisha ugonjwa hatari wa Covid-19.

Klabu zote 20 za EPL zilifanya kikao Jumatatu kwa lengo la kujadili mabadiliko ya ratiba, baada ya mechi sita za Ligi Kuu kuahirishwa wikendi iliyopita.Lakini klabu zilikubaliana ratiba iendelee lakini katika “mazingira salama”.

Kulikuwa na madai kwamba mechi za kombe la EFL – maarufu kama Carabao Cup – zingepigwa breki kuanzia Desemba 28 ili kuondolea wachezaji na klabu preshaLakini sasa imeafikiwa kwamba, klabu ikiunga kikosi cha wachezaji 13 walio fiti, pamoja na kipa mmoja, hawana budi ila kusakata mechi.

Hata hivyo, mechi za raundi ya tatu na nne za kombe lingine – FA Cup – zimeondolewa; huku mazungumzo vilevile yakiendelea kuhusu iwapo nusu-fainali za EFL Cup zitachezwa raundi moja badala ya mbili – nyumbani na ugenini.

Baada ya mkutano huo, wakuu wa ligi kuu walithibitisha kwamba asilimia 90 ya watu 12,345 waliofanyiwa vipimo kati ya Disemba 13 na Disemba 19 walipatikana na virusi vya Corona.Utafiti zaidi umeonyesha kwamba asilimia 77 ya wachezaji tayari wamepigwa chanjo la kuzuia ugonjwa huo kufikia Jumatatu.

Ripoti hiyo imeonyesha kuwa asilimia 84 ya wachezaji wa ligi kuu wamepata chanjo la kwanza huku wakingojea la pili, lakini wakijumuishwa na maafisa wao wa kiufundi, idadi hiyo inapanda hadi asilimia 92.Kulipuka upya kwa Corona ulisababisha kutolewa kwa mechi kadhaa ikiwemo ya Jumamosi kati ya Aston Villa na Burnley dakika ya mwisho.

Jumapili, Chelsea na Wolves zilicheza bila wachezaji wao kadhaa wa kutegemea ambao ripoti zao zilikuwa zikisubiriwa. Kadhalika, Liverpool ilikabilaiana na Tottenham bila mastaa kadhaa wa kikosi cha kwanza.Mechi sita ziliahirishwa Jumamosi, huku juhudi za Chelsea kutaka mechi yao na Wolves itolewe zikikambulia patupu.

Baada ya Carabao Cup zitakazochezwa Disemba 21 na Disemba 22, kuna timu zitakazorejea uwanjani kucheza mechi tatu za EPL kuanzia wakati huo hadi Januari 2.

You can share this post!

CECIL ODONGO: Mudavadi ataingia ikulu rahisi kupitia kwa...

Raga: Vidume wa Shamas RFC bado juu ligi ya kitaifa

T L