Michezo

KIZAAZAA: Fataki Emirates Arsenal wakitoana kijasho na Napoli, Chelsea ugenini

April 11th, 2019 3 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KLABU mbili maarufu, Arsenal na Napoli leo Alhamisi usiku zitakutana ugani Emirates katika mechi ya mkondo wa kwanza ya kuwania nafasi ya kufuzu kwa nusu-fainali ya dimba la Europa League.

Kwenye mechi nyingine ya haiba kubwa, Chelsea inatua jijini Praque, Jamhuri ya Czech kukabiliana na Slavia Prague.

Arsenal walitinga robo-fainali kwa shida baada ya kutatizika katika mechi mbili za kufuzu, lakini ilikuwa kazi rahisi kwa wapinzani wao, Napoli ambao waliandikisha ushindi dhidi ya FC Zurich na Red Bull Salburg.

Katika hatua ya 32 bora na 16 bora, Arsenal walishindwa katika kila mechi ya mkondo wa kwanza na BATE Borisov na pia Rennes, kabla ya kujiimarisha kushinda marudiano.

Vijana hao wa kocha Unai Emery wangali katika kinyang’anyiro cha kumaliza miongoni mwa nne bora, licha ya majuzi kuteremka hadi nafasi ya tano jedwalini katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), nyuma ya Chelsea.

Baada ya kuendeleza rekodi yao ya kutoshindwa nyumbani kufuatia ushindi wa 2-0 dhidi ya Newcastle United, matumaini yao yalipunguzwa kufuatia kichapo cha 1-0 kutoka kwa Everton.

Baada ya Chelsea kuilaza West Ham United 2-0 na kusonga hadi nafasi ya tatu, itabidi Arsenal wajitahidi zaidi katika mechi zilizobakia ili warejee katika mduara wa kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), msimu ujao.

Iwapo watamaliza ligi nje ya nne bora, watajilaumu wenyewe kwa kuwa wamekuwa katika kiwango bora msimu huu, huku wakiandikisha ushindi mara 14 katika mechi 17 za ligi nyumbani, ikiwemo ushindi mara 10 mfululizo.

Sharti waandikishe ushindi hapa nyumbani ili kuwa na kazi rahisi watakapokuwa ziarani ugani Stadio San Paolo kwa mkondo wa pili.

Kwa upande mwingine, Napoli sio timu ya kudharau baada ya hapo awali kupangwa katika kundi moja na miamba PSG, Liverpool na Red Stars Belgrade na kumaliza katika nafasi ya tatu, licha ya kupoteza mechi moja pekee.

Kocha wao, Carlo Ancelotti amesema wana haja ya taji la Ulaya, hivyo watacheza kwa kujitolea zaidi ya uwezo wao.

Walibanduliwa katika hatua ya nusu-fainali msimu wa 2014-15, muongo mmoja na nusu (1988-89) baada ya kuibuka mabingwa, nyota mstaafu Diego Maradona akiwa kikosini.

Wanaingia uwanjani baada ya kuchapwa na Empoli 2-1 juma lililopita katika mechi ya Serie A na baadaye kuagana 1-1 na Genoa, Jumapili, huku wakiachwa kwa mwanya wa pointi 20 na vinara Juventus.

Jijini Prague, Chelsea wanatarajiwa kushinda SK Slavia Prague katika pambano la robo-fainali la mkondo wa kwanza la Europa League.

Katika mechi hiyo itakayochezewa ugani Sinobo, vijana hao wa kocha Maurizio Sarri wanwekewa nafasi kubwa ya kushinda kutokana na kiwango chao cha sasa.

Lakini hawatapata mteremko dhidi ya wapinzani wao ambao awali waliibandua nje Seville 3-2 katika hatua ya kufuzu kwa roboa-fainali.

Baada ya kumvutia kocha, huenda kinda Callum Hudson-Odoi akajumuishwa kikosini, baada ya kupewa nafasi katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Brighton na West Ham United.

Nyota huyo wa timu ya taifa ya Uingereza ameanza kucheza kwa kiwango cha juu, kiasi cha kuanza kutegemewa badala ya akina Pedro na Willian ambao wamekuwa wakicheza nafasi hiyo.

Pigo

Kwa upande mwingine wenyeji, Slavia Prague watakuwa bila Tomas Soucek ambaye kwa sasa amepigwa marufuku.

Kadhalika kikosi hicho kina wachezaji watano ambao wameonyeshwa kadi ya njano. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Chelsea kukutana na Slavia Prague.

Hata hivyo, wenyeji wamewahi kucheza na timu za Uingereza awali mara tisa, wakishinda mara moja tu 1-0 dhidi ya Leeds United mnamo 2000.

Chelsea kwa upande wao, wamewahi kuzuru Prague kabla ya pambano hili, wakicheza na Sparta na kushinda 1-0 katika mikondo yote, majuzi kabisa ilikuwa mnamo 2013 walipotwaa ubingwa wa taji hili wakiwa chini ya kocha Rafa Benitez.

Watakuwa wanaingia uwanjani wakijivunia ushindi wa majuzi wa 2-0 dhidi ya West Ham United, wakati Prague wakiwa na rekodi ya kutoshindwa katika mechi 10 msimu huu, na mabao 17 katika mechi tano.

Chelsea itakuwa na Arrizabalaga; Zappacosta, Rudiger, Luiz, Alonso; Kante, Jorginho, Kovacic, Pedro, Giroud, Willian.

Kikosi cha Slavia Prague kitakuwa na: Kolar; Kudela, Ngadeu-Ngadjui, Deli; Masopust, Traore, Zmrhal, Kral, Boril; Stoch, Skoda.