Habari Mseto

Kizaazaa mahabusu wakipigania pesa za wizi

September 7th, 2018 1 min read

Na Titus Ominde

KULITOKEA kizaaza katika seli ya mahakama ya hakimu mjini Eldoret pale mahabusu walipozozania Sh5,000 ambazo walidaiwa kunyang’anya mahabusu mwingine wa kike.

Kizaazaa hicho kilianza pale mahabusu wahusika walipokosa kuafikiana namna ya kugawana pesa hizo.

Baada ya kushindwa kuafikiana kuhusu namna ya kugwana pesa hizo, walianza kurushana makonde huku wakisababisha msukumano wa vishindo katika seli hiyo.

“Wewe huwezi ukachukua pesa nyingi ilhali mimi ndiye niliyemnyang’anya, kama ni hivyo acha turudishie mwenyewe,” sauti ilisikika katika seli.

Kizaazaa hicho kilifanya hakimu mkuu wa Eldoret, Bw Charles Obulutsa akimbilia katika seli hiyo ili kujua kilichokuwa kikiendelea.

Hatimaye maafisa wa usalama katika mahakama hiyo waliingilia kati na kuwapa washukiwa ambapo walinyang’anywa pesa hizo na kurudishiwa mwenyewe huku mahabusu waliomnyang’anya wakifunguliwa mashtaka mengine ya wizi wa mabavu wakiwa katika seli ya mahakama.

Hata hivyo maafisa hao walilaumu mama ambaye alinyang’anywa pesa hizo kwa kuingia nazo katika seli badala ya kuapatia maafisa wa usalama wa mwekee.