HabariSiasa

Kizaazaa Miguna kuzuiwa JKIA akitoka Canada

March 26th, 2018 1 min read

Na WANDERI KAMAU

KIZAAZAA kilizuka Jumatatu katika Uwanja wa Kitaifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) baada ya maafisa wa Idara ya Uhamiaji kumzuilia wakili Miguna Miguna aliyewasili nchini.

Bw Miguna aliwasili katika uwanja huo mwendo wa saa nane mchana kama alivyopangiwa, ila hakuruhusiwa kuondoka mara moja, “hadi pale angetimiza kanuni fulani.”

Muda mfupi baada ya kufika, maafisa hao walimtaka Bw Miguna kutia saini stakabadhi fulani na kusalimisha paspoti yake ya nchi ya Canada, ila mawakili wake walisema walimwonya dhidi ya kufanya hivyo.

Kulingana na wakili wake, Nelson Havi, huo ni mpango wa serikali kumpa visa ya muda ili kumfanya kuupoteza uraia wake baada ya miezi sita.

“Tumemwagiza mteja wetu dhidi ya kutia saini stakabadhi zozote, kwani njama iliyopo ni ya kumpa stakabadhi ya muda, ili kumnyang’anya uraia wa Kenya, ili serikali imrejeshe Canada tena baada ya kipindi cha miezi sita kuisha,” akasema Bw Havi.

Na hadi tukienda mitamboni, Bw Miguna alikiuwa angali anazuiliwa katika uwanja huo.

Bw Miguna alirudishwa ghafla nchini Canada mwezi uliopita, baada ya kuzuiliwa kwa siku tano na polisi kwa kumlisha kiapo kinara wa Nasa Raila Odinga kama ‘Rais wa Wananchi’ mnamo Januari 30.

Tangu kurejeshwa nchini humo, amekuwa akihutubia vikao katika miji mbalimbali katika nchi za Amerika na Canada, ambako amekuwa akiilaumu serikali ya Jubilee kwa ‘kumhangaisha’ bila sababu.

Bw Miguna pia amekosoa vikali muafaka wa kisiasa kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta, akiutaja kutokuwa suluhisho kwa changamoto zinazoikabili nchi.

Aidha, alimlaumu Bw Odinga kwa “kuwasaliti” wafuasi wake kwa hatua yake kukubali kuingia katika muafaka huo.