Habari Mseto

Kizaazaa mwanamke kuvua nguo kortini baada ya hukumu

February 21st, 2018 1 min read

Na GERALD BWISA

MWANAMKE wa miaka 28, Jumanne alizua kizaazaa katika mahakama moja ya Kitale baada ya kuvua nguo akilalamikia kifungo cha miezi sita alichopewa kwa kosa la kumshambulia jamaa yake.

Mshtakiwa, Robinah Mwanja, ambaye ni mama wa watoto watano alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Dorcas Wangeci, ambapo alishtakiwa kufanya kosa hilo mnamo Desemba 1, 2017.

Alishtakiwa kumshambulia shemejiye, Bridgit Nanjala katika Shamba la Meso, Kaunti ya Trans Nzoia ambapo alimjeruhi.

Aidha, mshtakiwa alikubali mashtaka hayo, ambapo aliiomba mahakama kumsamehe, kwa kisingizio kwamba alikuwa akijizuia dhidi ya kushambuliwa na mlalamishi. Hata hivyo, kizaazaa kilianza baada ya kusomewa kifungo chake.

Mshtakiwa alimrusha mtoto wake wa miezi sita chini ambaye alikuwa amemshikilia, ila kwa bahati nzuri akashikwa na Msamaria Mwema kabla yake kuanguka.

 

‘Siendi jela’

“Huko jela siendi ng’o!” akasema, huku akivua nguo zake.

Hata hivyo, polisi waliokuwa karibu walifaulu kumpeleka katika gari lilolokuwa karibu, ambapo alisafirishwa katika Gereza la Serikali la Kitale ili kuanza kifungo chake.

Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa mshtakiwa kufikishwa mahakamani, kwani. Mnamo Mei mwaka uliopita, alikamatwa kwa kuwatelekeza watoto wake.

Kulingana na mlalamishi, mshtakiwa alimkuta nyumbani kwa ndugu yake (ambapo mshtakiwa alikuwa akikaa baada ya kuachana na mumewe).

“Tulianza mabishano kuhusu kuni. Mvutano huo ulimfanya kuchukua jiwe na kunigonga usoni ambapo nilianza matatizo ya kula,” akasema Bi Nanjala.
Aliiomba mahakama kutompa kifungo cha nje, kwani anaamini kwamba hilo huenda likamoa nafasi ya kumshambulia tena.