Habari Mseto

Kizaazaa nyumba ikibomolewa Viwandani

January 21st, 2020 1 min read

Na SAMMY KIMATU

KULIKUWA na sinema bila malipo katika eneo la Express kando ya barabara ya Likoni katika kaunti ya Nairobi Jumanne asubuhi.

Haya yalitokea wakati diwani wa wadi na mkuu wa tarafa walibomoa nyumba iliyojengwa na wanyakuzi wa ardhi juu ya bomba la maji.

Mwakilishi wa wadi ya Land Mawe, Bw Herman Azangu Kaimosi na Msaidizi wa Kamishena wa Kaunti ya South B, Bw Philip Mbuvi walijihami kwa nyundo.

Aidha, wawili hao waliwaongoza vijana katika kukurukakara za kubomoa kibanda hicho.

Bw Azangu aliwalaumu wanyakuzi wa ardhi kwa kujenga nyumba juu ya mtaro wa kupitisha maji machafu kando ya daraja la Express.

Wakazi waliwalaumu chifu, naibu wake na wazee wa mitaa wakidai wameuza ardhi kwa mwenyekiti wa mtaa mmoja kwenye maeneo hayo.

Mmilii wa nyumba hiyo alipotea alipopashwa habari wa wadokezi wake.

“Ni aibu na haikubaliki kwa mtu kunyakua kingo za mto. Mijengo yote iliyojengwa karibu na mto wa Ngong itabomolewa na tingatinga hivi karibuni.

“Mwanamume huyu anamiliki nyumba nyingi zinazohatarisha maisha ya watu kando ya mto na bado watu wanakodi bila kuogopa maisha yao, ” Bw Mbuvi akasema.

Wanyakuzi wa ardhi ni maarufu kando ya mto Ngong na wengine wamepanga magunia ya mchanga na kujenga nyumba juu yake.

Katika tukio hilo, nyumba kadhaa zilizojengwa karibu na mto nusura zitumbukie mtoni Ngong wakati mvua ilinyesha zaidi mwezi Desemba.

Nyumba hiyo, ilikuwa na vyumba vya kukodisha na maduka lakini tangu wakati huo, watu wote walitoka kwa hofu ya maisha yao.

Mmiliki wa jengo ameondoa mabati yaliyoiezeka.