Michezo

KIZAAZAA OLD TRAFFORD: Manchester United na City kupapurana Jumapili

March 7th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

MAJOGOO wa jiji la Manchester, United na City, watapapurana Jumapili kwa mara ya nne msimu huu katika debi kali ya Manchester.

Vijana wa Pep Guardiola, Man-City watafunga safari ndogo ya kilomita sita hadi uwanjani Old Trafford kwa debi yao ya 28 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Man-United wako nambari tano kwenye ligi kwa alama 42. Tayari wamepepeta nambari mbili, Man-City mara mbili msimu huu uwanjani Etihad.

Vijana hao wa kocha Ole Gunnar Solskjaer walichabanga mabingwa hao watetezi wa EPL mabao 2-1 kupitia mikwaju ya Marcus Rashford na Anthony Martial mwezi Desemba.

Kisha wakawanyuka 1-0 kwa bao la Nemanja Matic kwenye mechi ya marudiano ya nusu-fainali ya kombe la League Cup, mwezi Januari.

Man-United, ambayo iko katika orodha moja na Wolves, Tottenham, Sheffield United, Burnley, Arsenal na Everton kuwania tiketi ya nne ya kuingia Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), itakuwa ikisaka ushindi wake wa kwanza dhidi ya Man-City uwanjani Old Trafford katika mechi nne.

Man-City, ambayo ina alama 57 , ililaza Man-United magoli 2-0 mwaka 2019 ligini kabla kuilima 3-1 Januari mwaka huu kwenye mechi ya mkondo wa kwanza ya nusu-fainali ya League Cup uwanjani humu.Man-United itang’oa Chelsea katika nafasi ya nne iwapo itapiga Man-City nao vijana wa Frank Lampard wapoteze dhidi ya Everton, uwanjani Stamford Bridge kesho Jumapili saa kumi na moja jioni.

Solskjaer atakosa huduma za kiungo Paul Pogba na mshambuliaji Rashford wanaouguza majeraha. Kuna uwezekano mkubwa pia hatakuwa na beki Harry Maguire aliyepata jeraha la kifundo dhidi ya Derby County, katika mechi ya raundi ya tano ya Kombe la FA siku ya Alhamisi. Man-United ilishinda mchuano huo 3-0 kupitia mabao ya Odion Ighalo (mawili) na Luke Shaw. Beki Aaron Wan-Bissaka na kiungo Daniel James huenda pia wakakosa debi ya Manchester. Mshambuliaji Sergio Aguero ataongoza safu ya mashambulizi ya Man-City akishirikiana na Raheem Sterling. Aguero amefunga mabao 11 dhidi ya mahasimu wao wa kesho. Atakaribia rekodi ya magoli 11 ya gozi hili inayoshikiliwa na Wayne Rooney.

Man-City huenda ikakosa huduma za kiungo Kevin De Bruyne aliyeumia bega katikati mwa juma.

Vilevile, Aymeric Laporte (beki) na Leroy Sane (fowadi) ambao wako mkekani wakiuguza majeraha.

Vikosi tarajiwa: Manchester United – David De Gea, Victor Lindelof, Harry Maguire, Luke Shaw, Aaron Wan-Bissaka, Fred, Nemanja Matic, Daniel James, Bruno Fernandes, Mason Greenwood, Anthony Martial.

Manchester City – Ederson, Kyle Walker, Nicolas Otamendi, Oleksandr Zinchenko, Benjamin Mendy, Rodri, Fernandinho, Kevin De Bruyne, Raheem Sterling, Sergio Aguero, Bernardo Silva.