Habari MsetoSiasa

Kizazi kipya cha 'Mamba' kitamzuia Raila kufika Canaan – Kiunjuri

March 9th, 2020 1 min read

Na JAMES MURIMI

ALIYEKUWA Waziri wa Kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri, amedai kuna kizazi kipya cha ‘mamba’ ambao watamzuia Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kuingia ikulu ifikapo 2022.

Bw Odinga amekuwa akitumia msemo wa mamba kwenye Mto Jordan kurejelea vikwazo vinavyotatiza maazimio ya Wakenya kuafikia maisha bora.

Akihutubu kwenye hafla moja ya mazishi katika Kaunti ya Laikipia mnamo Jumamosi, Bw Kiunjuri alisema uhusiano wa Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta hautamsaidia kwa vyovyote vile kutwaa nafasi hiyo.

“Raila amekuwa akisema mamba wametolewa katika Mto Jordani. Ni kweli, waliondolewa, lakini hao ni mamba wazee ambao hawawezi kushiriki kwenye vita vyovyote. Tayari, wamepelekwa katika kituo cha kuwahifadhi wanyama kwa kuwa wamechoka.

Tunataka kumhakikishia Raila kwamba hatavuka mto huo kwani mamba hao wapya wametulia kwa sasa. Ni wenye nguvu na wanaweza kushiriki kwenye vita,” akasema.

Alisema hayo kwenye mazishi ya Bi Perishina Muringo katika kijiji cha Mwireri, Kauti Ndogo ya Laikipia Mashariki.

Baadhi ya viongozi walioandamana naye ni aliyekuwa gavana wa Laikipia Bw Joshua Irungu, Seneta John Kinyua, Spika wa Bunge la Laikipia Bw Patrick Waigwa na madiwani kadhaa.