Habari Mseto

Kizimbani baada ya kunaswa na kontena ya nepi feki

January 31st, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYAKAZI wa kampuni ya Imperial Industrial Park Limited alishtakiwa kwa kuuza nepi feki za watoto.

Bw John Githinji Gichuhi alifikishwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi akikabiliwa na mashtaka ya kupatikana na kontena iliyojaa nepi feki.

Bw Gichuhi alikanusha mashtaka matatu dhidi yake na kuomba aachiliwe kwa dhamana.

Mahakama ilifahamishwa na kiongozi wa mashtaka Bi Kajuju Kirimi kuwa kesi dhidi ya Bw Gichuhi itaunganishwa na nyingine ambapo mshukiwa mwingine ameshtakiwa.

Korti ilielezwa Bw Gichuhi alikutwa katika mabohari yaliyoko eneo la Mlolongo, Kaunti ya Machakos akiwa na kontena iliyojaa mabunda 5094 ya nepi feki.

Shtaka lilisema nepi hizo hazikuwa zimewekwa alama ya siku ya kutengenezwa wala muda wa kuharibika.

Mshtakiwa huyo alidaiwa pia alikutwa  akifuta siku ya kutengenezwa kwa nepi hizo zenye nembo ya Ezee.

Bw Andayi aliombwa amwachilie mshtakiwa kwa dhamana.

“Sipingi mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana,” alisema Bi Kirimi.

Mahakama iliamuru mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana ya pesa taslimu Sh200,000 hadi Februari 28, 2019 kesi itakaposikizwa.