Habari Mseto

Kizimbani kwa kufuga kasuku kinyume cha sheria

May 13th, 2019 1 min read

Na BENSON MATHEKA

Mtaalamu wa afya ya wanyama jijini Nairobi, Jumatatu alifikishwa katika mahakama ya Kibera akikabiliwa na shtaka la kupatikana akifuga Kasuku kinyume cha sheria.

Ilidaiwa kwamba Bw Morris Munene alipatikana na ndege huyo mwenye thamani ya Sh30,000 katika eneo la Langata bila kibali kutoka kwa serikali.

Kulingana na mashtaka, Munene alitenda kosa hilo Mei 12 mwaka huu.

Bw Munene alikanusha mashtaka na kusema kwamba alipatiwa ndege huyo na mteja wake aliye na leseni ya kufuga ndege wa pori ili amtibu.

“Huyu sio ndege wa Shirika la Kulinda Wanyama Pori. Ni mali ya mtu binafsi aliye na leseni ya kumtunza,” Bw Munene aliambia mahakama upande wa mashtaka ulipoomba uruhusiwe kumrudisha ndege huyo msituni.

Alisema kazi yake ni kutibu wanyama pori na akaomba mahakama imwachilie kwa dhamana nafuu.

“ Ninategemea kazi ya kutibu wanyama kutunza familia yangu change na nikinyimwa uhuru wangu, watateseka,” alisema.

Hakimu Mwandamizi wa Kibera Boaz Ombewa alimwachilia kwa dhamana ya Sh30,000 pesa taslimu. Kesi itatajwa Januari 20 ili anayedaiwa kumiliki ndege huyo awasilishe leseni au akikosa kufanya hivyo arudishwe msituni kisha kesi iendelee.