Habari Mseto

Kizimbani kwa kuhadaa polisi alitolewa mimba alipotekwa nyara

January 9th, 2019 2 min read

Na BRIAN OCHARO

MWANAMKE wa miaka 20 ameshtakiwa katika mahakama ya Mombasa kwa kutoa taarifa za uongo juu ya ujauzito na utoaji wa mimba. Saida Abdulrahman Barak na mumewe Mohamed Abdulahman (pichani) walifikishwa mahakamani Jumanne na kushtakiwa kwa kutoa habari za uongo kwa polisi.

Bi Barak anashutumiwa kutoa taarifa za uongo kwa mhudumu wa afya Dkt Nafsa Mohamed katika Hospitali Kuu ya Mkoa wa Pwani kuwa alikuwa na mimba ya miezi minane na alikuwa amepoteza mimba hiyo katika mikono ya waliomteka nyara huko Malindi, Kaunti ya Kilifi mnamo Septemba 20, 2018.

Mwanamke huyo alishtakiwa baada ya ripoti ya matibabu kutoka CPGH kuthibitisha kuwa hawezi kubeba mimba na kwamba alikuwa amepoteza mimba Machi.

Hii ilikuwa kinyume na taarifa aliyowapa mapema polisi kwamba alikuwa mjamzito wa miezi minane mwezi wa Septemba wakati alitekwa nyara na kuachwa katika jiji la Nairobi.

Mwanamke huyo alidai kuwa watekaji nyara hao walimkamata wakati akielekea kuabiri matatu ya kuelekea Malindi katika kituo cha Buxton mjini Mombasa.

Mtuhumiwa alikuwa apande ndege ya mchana huko Malindi kuelekea Lamu wakati alidai kutekwa nyara na wanawake sita.

Kwa mujibu wa ripoti yake ya awali kwa polisi, mtuhumiwa alidai kuwa alitiliwa dawa kabla ya kutekwa nyara na kwamba baada ya kupata tena ufahamu, aligundua kuwa hakuwa mjamzito tena.

Mtuhumiwa aliwaambia wachunguzi kuwa alitoroka kutoka kwa mikono ya watekaji nyara wake katika chumba kimoja jijini Nairobi ambako alikuwa amewekwa na kukimbilia usalama ambapo aliokolewa na Msamaria mwema ambaye pia aliwasiliana na familia yake huko Nairobi.

Mume wa mwanamke huyo Abdulahman pia alishtakiwa kwa kutoa trifa za uongo kwa polisi kuhusu utekaji nyara wa mkewe ambaye alidai ni mjamzito.

Mtuhumiwa huyo anashtakiwa kwa kumuambia Konstebo wa Polisi Cyrus Mbugua, kwamba mkewe ambaye alikuwa mjamzito wa miezi minane alipotea baada ya kumwambia mama yake Hadija Bwana kwamba alikuwa safarini kueleke Lamu.

Kwa mujibu wa wapelelezi, mtuhumiwa alijua au aliamini kwamba taarifa aliyokuwa ametoa yalikuwa ya uongo, na hivyo kumfanya afisa wa polisi kuanzisha shughuli za kumtafuta Bi Barak.

Watuhumiwa walikanusha makosa wanayoshtakiwa kufanya mnamo Septemba 20 na 24, mwaka jana, katika hospitali ya CPGH na kituo cha polisi cha Makupa wakati walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Christine Ogweno.

Watuhumiwa kupitia kwa wakili wao Khalid Salim walitaka kupewa dhamana ya chini wakidai hawawezi kutoroka na kuwa wana mahali pa kudumu ya makazi.

“Watuhumiwa kwa hiari walikuja mahakamani baada ya kupewa dhamana ya polisi ya Sh10,000 kila mmoja , hii ni dhihirisho kwamba hawawezi kuhepa. Wako tayari kuhudhuria mahakama wakati wowote wanapohitaji kufanya hivyo, “alisema

Bw Khalid alisema mashtaka hayo ni madogo na kwamba mashahidi wa msingi ni maafisa wa polisi hivyo hakuna wasiwasi watuhumiwa wanaweza kuingilia kati mashahidi.

Watuhumiwa hao waliachiliwa kwa dhamana ya Sh100,000 kila mmoja na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho.

Kesi hiyo itatajwa tena Januari 24.